Kazi ya tafsiri haifanywi kiholela bali
huzingatia baadhi ya hatua ili kufikiwa kiufanisi. Kwan kumrejelea Mwansoko
(2006), anabainisha hatua zifuatazo:
Kwanza, mfasiri akabiliwapo na matini ya
sayansi na teknolojia kwanza aisome kwa makini ili kuelewa maudhui yake. Lengo
ni kufanya matini lengwa iakisi matini chanzi kiujumbe, zaidi ni kupigia
mistari katika maneno magumu ili kuweza kuyatafutia maana katika vyanzo
mbalimbali kama vile, kamusi ili kufanikisha zoezi la tafsiri.
Pili, ni kutathimini ubora wake. Mfasiri anapaswa kuchunguza ubora wa matini
chanzi, ili kuangalia kiwango chake cha urasimi yaani umaalumu kwa mfano;
istilahi zilizotumika ni za kisayansi, mifano iliyotolewa inahalisika
kisayansi, au mambo yanayoongelewa ni ya kisayansi. Jumla ya mambo haya
yanatakiwa kuzingatiwa na mfasiri kwani yanathibitisha uhai wa matini ya kiufundi.
Tatu, baada ya kuchambua matini yako
ifasiri hasa kwa mkabala wa sentensi kwa sentensi. Mkabala huu unasisitizwa
kwani unaeleweka zaidi kuliko wa neno kwa neno ambao kimsingi huweza kutuletea
maana tenge katika tafsiri.
Nne, iweke tafsiri yako katika umbo
linalotakiwa na mteja wako. Mfano; kama unafasiri kwa ajili ya shirika fulani
la uchapishaji fuata mtindo wa machapisho ya shirika hilo kwa kuzingatia
machapisho ya awali, na kama unafasiri gazeti au jarida fuata mtindo wa uandishi
wake.
Baada ya kuangalia hatua za kufuata
katika kufasiri matini za kisayansi na teknolojia, ufuatao ni mtindo wa lugha
ambao mara nyingi hutumika katika kufasiri matini hizo:
Mwansoko (1994) na (2006), ameonesha
mtindo wa lugha unaotumika katika tafsiri ya kiufundi (sayansi na teknolojia).
Kwa kawida, lugha inayotumika katika tafsiri ya kiufundi huwa na lengo la
kueleza usahihi na ukweli wa mambo yanayojadiliwa. Hivyo nia ya mwandishi hapo
sio kusisimua au kuibua hisia au maono ya wale wanaomsoma au kumsikiliza, bali
ni kutoa taarifa tu kama ilivyo. Lugha inayotumika katika tafsiri ya kiufundi
kwa kawaida haina mhemko au jazba, ni ya msimamo wa katikati. Kutokana na sifa
hizo tunapata mambo yafuatayo:
Hutumia sana kauli za kutendwa. Kauli
hizi hutumika sana hata kama mwandishi ameandika kazi yake peke yake. Hii
hutumika ili kuondoa dhana ya umilikishi katika uga wa taaluma.
Mfano;
Masuala yaliyopendekezwa,
Jambo lililojadiliwa,
Imedhihirishwa,
Inapendekezwa,
Imekubaliwa n.k.
Jambo jingine ni matumizi makubwa ya
vitenzi vya kidhahania. Vitenzi hivyo vya kidhahania ni vile ambavyo havioneshi
au kubainisha waziwazi nafsi ya mtenda/mtendwa ama kubainisha mhusika. Matini
za sayansi na teknolijia hazioneshi umiliki kama zifanyavyo za taaluma zingine
kama fasihi.
Mfano;
Kutembelea vikundi mbalimbali vya
sanaa,
Kusoma tafsiri,
Ukimwi unaua chukua tahadhari.
Vilevile, ina matumizi makubwa ya nafsi
ya kwanza wingi mahali pa nafsi ya kwanza umoja. Mtindo wa lugha katika tafsiri
matini za kiufundi hukwepa matumizi ya nafsi ya kwanza umoja na badala yake
hutumia nafsi ya pili wingi ikiwa na lengo la kufanya watumiaji wa matini ile
kuamini kuwa imefanywa na watu wengi.
Mfano; Katika
sura inayofuata tutachambua kwa undani zaidi mtindo wa kirasimi...
Mwansoko (1994:26)
japo kitabu hichi kakiandika mwenyewe lakini katumia wingi.
Tunakubaliana na mawazo ya….
Tunazungumzia….
Kadhalika,
hutumia sana kauli zisizoonyesha nafsi ya mtendaji. Hii inajidhihirisha pale
ambapo mwandishi anakua kama amejitoa katika matini Fulani na kuonekana si
muhusika kwa kuweka baadhi ya vipashio ambavyo havioneshi nafsi dhahiri. Hivyo
tafsiri ya matini za kiufundi huwa na sifa hiyo.
Mfano,
Imeafikiwa kuwa
Imeadhimiwa kwamba
Ilipendekezwa yafuatayo
Inatazamiwa kwepo na…
Baada ya kuangalia mtindo wa lugha
unaotumika katika matini za sayansi na teknolojia, sasa tuangalie sifa bainifu/upekee
wa matini za sayansi na teknolojia kama ifuatavyo:
Kwanza, hazijigezi na utamaduni wowote.
Hii ni kwa sababu matini hizi hutarajiwa kutumiwa na watu wote/ulimwengu mzima
na hii ndio maana mara nyingi katika matini za kisayansi majina au istilahi
huandikwa kama yalivyo bila kujali athari zake/ukali wa maneno hayo kwa
utamaduni wa jamii fulani. Kwa mfano sehemu za mwili wa bianadamu mathalani
uke, uume, puru, korodani nakadhalika huandikwa bayana bila kujali nani
anapelekewa matini hizo, ana umri gani, heshima gani, au yuko katika muktadha
upi. Mfano mzuri tunaweza kurejelea katika vitabu vya sayansi shule za msingi
(darasa la sita) ambapo kuna michoro inayobainisha sehemu mbalimbali za mwili
wa mwanadamu. Halikadhalika katika zana mbalimbali za kiufundi mfano katika
karakana kuna kifaa kinachojulikana kama Mult-purpose
spanner ambacho kwa Kiswahili kimetafsiriwa kama spana malaya. Hivyo kwa
kiasi fulani kulingana na utamaduni wa waswahili kuna ugumu fulani katika kuzitaja
au kuzirejelea zana au vifaa tajwa hapo juu, na wengine huona kuwa ni matusi.
Tafsiri za matini ya sayansi na
teknolojia ina matumizi makubwa ya istilahi. Msokile, (1993) anaeleza kuwa,
istilahi ni neno litumikalo kwa ufupi wa maneno mengi ya kiufundi kufuatana na
ujuzi ama elimu maalumu. Kwa mfano, istilahi za fasihi, istilahi za kemia na
jiografia. Katika uga wa sayansi kuna istilahi mbalimbali kama ifuatavyo:
Istilahi za Hisabati ni sphere, triangle, pai na algebra.
Istilahi za Baiolojia ni genetic, photosynthesis, nutrition na excretion.
Istilahi za Kemia ni calcium, element, potassium na carbonate.
Istilahi za Fizikia ni electric, current, ampere na voltage.
Katika istilahi, huwa kuna ugumu katika kupata au kutambua maana za
istilahi mpya kwa mfasiri hasa zile ambazo hazifungamani sana na muktadha na
hutokea mara moja tu katika matini. Mkabala ulio bora zaidi kwa matini ya
kiufundi yenye istilahi nyingi za uvulivuli, ni kupigia mistari istilahi
zinazoonekana kuwa ni za msingi wakati usomapo matini chanzi kwa mara ya kwanza
na kisha tafuta maana zake kwenye kamusi. Istilahi hizo zinaweza kuwa na maana
zaidi ya moja katika Nyanja moja ileile.
Wakati
mwingine yawezekana ukakosa kabisa visawe vya istilahi za lugha chanzi katika
lugha lengwa yako. Hali hii inapotokea mfasiri hulazimika kuunda istilahi zake
mwenyewe kwa kutumia mbinu ambazo hutumiwa na lugha zote kuzalisha maneno
mapya. Mbinu hizo ni pamoja na kutumia lugha lengwa yenyewe kwa minyumbuliko,
miambatano, miungano, upanuaji wa maana za maneno yaliyopo na
uhulutishaji. Vilevile, mbinu ya kukopa
kutoka lugha nyinginezo, lahaja, istilahi za kimataifa pamoja na tafsiri sisi.
Upekee wa mwingine wa tafsiri za
kiufundi au za kisayansi na teknolojia, kwa kawaida huwa katika umbo la ripoti
ya kiufundi, lakini yawezekana pia ikajumuisha vitabu vya rejea, maelekezo au
notisi zinazoandikwa kwa kufuata mtindo wa maandiko ya kitaaluma. Hivyo upekee
huu ndio unaoitofautisha matini ya kisayansi na matini zingine ambazo si za
kisayansi. Na sifa hii ndiyo huweza kuitofautisha na matini nyingine kama za
kifasihi, kisheria, kidini na zingine ambazo zinakuwa katika umbo la sentensi
au katika aya ndefu, zisizokuwa katika mwonekano wa chati, grafu, orodha
vielelezo, picha kama ilivyo katika ripoti. Hili limeshadadiwa katika ukurasa
unaofuata. Pia, katika hoja ya kujumuisha vitabu vya rejea, kama kamusi, orodha
ya istilahi na marejeo mengine ni muhimu katika tafsiri ya kiufundi kwa sababu
kuna baadhi ya istilahi zinakuwa na maana zaidi ya moja. Kwa hiyo ni vyema
kurejelea katika marejeo ili kupata maana mahususi ya istilahi inayoendana na muktadha
husika. Kwa mfano; rejeleo lililoambatanishwa katika ukurasa unaofuata. Lakini
pia mara nyingine, matini hizi za kiufundi huweza kuwa tu katika mfumo wa notisi
au maelekezo ya kitaaluma kama vile, vitabu vya Baiolojia, Kemia, Jografia na
taaluma zingine za kisayansi.
Upekee mwingine ni kuwa, tafsiri ya
matini za kisayansi na teknolojia hutumia rejesta mbalimbali pamoja na
kuonekana imeandikwa vibaya. Rejesta ni mtindo wa lugha inayotumika mahali
penye shughuli maalumu inayotumiwa na kundi maalumu la wanajamii. Matumizi ya
rejesta nyingi katika tafsiri hii hutokana na tafsiri hii kuwa na mada nyingi
tofauti na tafsiri nyingine. Mfano katika vitabu vingi vya sayansi huwa na mada
nyingi zilizochambuliwa tofauti na vitabu vya sanaa kama fasihi. Vilevile
rejesta nyingi hutokana na mazoea ya watumiaji kama vile, mafundi magari,
mafundi baiskeli, watu wa uhandisi na wengine. Kwa mfano fundi baiskeli hutumia
rejesta kama vile;
Siti kava – kumaanisha
sehemu anayokaa anayeendesha baiskeli
Stelingi – kumaanisha
usukani
Breki – vifaa vya
kufunga ili kupunguza mwendo
Sahanipeda – kifaa kama
sahani ambacho hushika mnyororo
Medigadi – kifaa cha
kukinga tope kinachopatikana katika gurudumu
Tairi – gurudumu
breki filiwili kiti stelingi
spoku
Tairi (gurudumu)
gia padeli
Rejesta na maneno yaliyofasiriwa hapo
juu ni ya kisayansi na mwonekano wake na namna yanavyosikika katika lugha ya
Kiswahili yanaonekana kutokuwa vizuri (hayavutii). Siyo hayo tu, pia hata
katika simu tunazozitumia tafsiri ya maneno kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili
zinaonekana kuwa na ukakasi huo huo uliojitokeza hapo juu. Kwa mfano;
Setting – mipangilio
Phone book – majina
Profile – mifumo
Alarm – kengele
Torch
– taa
Images – picha
Sms
– ujumbe
Hiyo ni kwa mujibu wa shirika la simu
linaloitwa Nokia.
Kwa
kuhitimisha tunaweza kusema kuwa, tafsiri ya sayansi na teknolojia ina
upekee sana japo inakabiriwa na changamoto mbalimbali kama vile, ugumu wa
upatikanaji wa istilahi za kisayansi na ugumu wa kupata maana za maneno au
istilahi hizo za kisayansi na teknolojia. Hivyo changamoto hizo zinaleta shida
katika tafsiri ya matini za sayansi na teknolojia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni