Ijumaa, 9 Januari 2015

KATEGORIA ZA KISARUFI KWA MKABALA WA KIMAPIKEO

 KATEGORIA ZA KISARUFI KWA MKABALA WA KIMAPIKEO



Dhana ya kategoria ya kisarufi ni dhana telezi na ina ukakasi katika kuieleza licha ya uwepo wa  wataalamu mbalimbali ambao wamejaribu kuifasili. Katika kujibu swali hili tutaanza kueleza maana ya kategoria jinsi ilivyoelezwa na wataalamu mbalimbali, tutaeleza maana ya kategoria ya kisarufi, vilevile tutaelezea dhana ya sarufi mapokeo tukihusisha mawazo ya wataalamu  mbalimbali, pia tutadadavua kategoria ya kisarufi kwa mkabala wa sarufi mapokeo hatimaye tutahitimisha kwa kueleza faida na hasara za sarufi mapokeo.
Kwa kuanza, tuijadili dhana ya kategoria ya kisarufi jinsi ilivyojadiliwa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo;
Zabroni (2013); anaeleza kuwa, kategoria ni sifa zinazoambikwa katika aina mbalimbali za maneno.
Chombozi. Blogspot.com; waeleza kuwa, kategoria ni aina za maneno kadri ya uainisho wake kutegemeana na sifa za maneno husika kuwekwa katika kundi moja.
Matinde (2012); wanaeleza kuwa, kategoria ni jumla ya maumbo, faridi na vipashio vilivyo katika hadhi sawa  na huchangia sifa fulani katika tungo.
Hivyo, tunaweza kueleza kuwa kategoria ni maumbo au vipashio mbalimbali vya kisarufi vinavyotumika kubainisha mahusiano ya maneno katika tungo mbalimbali za lugha.
Baada ya kupata uelewa juu ya dhana ya kategoria kama ilivyoelezwa na wataalamu mbalimbali, sasa tujadili dhana ya kategoria ya kisarufi huku tukihusisha mawazo yetu na mawazo ya  wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo;
www.out.ac.tz; wanaeleza kuwa, kategoria ya kisarufi ni kundi la maneno lenye sifa za kisarufi zinazofanana.
Matinde  (2012: 187);  anaeleza kuwa, kategoria za kisarufi ni maumbo au vipashio vya kisarufi vinavyotumika kubainisha mahusiano ya kategoria za maneno katika sentensi.
www. Englishclub.com;  wanaeleza kuwa, kategoria za kisarufi (grammatical category) inahusu sifa maalumu ya neno ambayo inaweza kusababisha kwamba neno au maneno  kuhusiana na mabadiliko katika mfumo wa kisarufi. ( tafsiri yetu)
www.thefreedictionary.com;  wanaeleza kuwa, kategoria za kisarufi ni aina za maneno yenye sifa za kisarufi zinazofanana.
Kwahiyo tunaweza kusema kwamba, kategoria za kisarufi ni sifa ya kitu (maneno au neno) ndani ya sarufi ya lugha.
Baada ya kueleza maana ya kategoria ya kisarufi jinsi livyoelezwa na wataalamu mbalimbali na vyanzo vingine. Sasa tuieleze dhana ya sarufi mapokeo huku tukihusisha mawazo ya wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo;
Massamba na wenzake (1999); wanafafanua kuwa sarufi mapokeo ni sarufi elekezi ilisisitiza usahihi wa lugha kwa kuonyesha sheria ambazo hazina budi kufuatwa, mathalani, kufanya muundo fulani wa sentensi uonekana  kuwa sahihi, au sheria ambazo hazina budi kufuatwa  ili kufanya matamshi ya neno fulani yakubalike kuwa ndio sahihi. Sarufi  hizo za kimapokeo zilikuwa zikisisitiza jinsi ambavyo lugha haikupaswa kuwa.
Kwahali hiyo; tunaweza kusema kuwa, sarufi mapokeo  ni sarufi ya kale  ambayo ilionekana kutokuwa na msimamo wa Kisayansi katika kuelezea lugha bali ilikuwa na mwelekeo wa kifalsafa na kujikita katika kutambulisha kategoria mbalimbali za kisarufi ambazo zinatumika hadi hivi sasa.
Baada ya kumaliza kujadili maana ya sarufi mapokeo;  sasa tuzigeukie kategoria za kisarufi kwa mujibu wa mkabala wa sarufi mapokeo ,
Kategoria ya nafsi; hii ni kategoria ya sarufi mapokeo ambayo huelezea viwakilishi vya matenda/ mtendwa ambavyo huambikwa kwenye vitenzi.Jedwali lifuatalo linaoneshsa  kategoria za nafsi tatu ambazo pia zinaonekana katika maumbo ya umoja na wingi zikiwa na viambishi vipatanishi vyake.
Nafsi
Umoja
Viambishi vipatanishi
Wingi
Viambishi vipatanishi
   I
Mimi
        Ni-
Sisi
            Tu -
   II
Wewe
         U -
Ninyi
           M -
   III
Yeye
        A -
Wao
           Wa -
Mfano wa utokeaji wa nafsi katika tungo;
(i)                 Ni-, hii huonesha nafsi ya kwanza .
 Mfano; Mimi ninakula.  (umoja)
              Sisi tunakula.  (wingi)
(ii)               U-,  hii huonesha nafsi ya pili .
(iii)             Mfano: Juma unakula? (umoja)
                Juma mnakula? (wingi)
(iv)             A-, hii hueonesha nafsi ya tatu .
   Mfano: Mtoto anakimbia. (umoja)
                Watoto wanakimbia. (wingi)
Kategoria ya njeo. ni kategoria ya kisarufi mapokeo ambayo huonesha na kuelezea tendo linavyotendeka ,lilivyotendeka na litakavyotendeka. Katika lugha ya Kiswahili kategoria za njeo huwakilishwa na viambishi vitatu ambavyo ni;  -na-,  -li-, na –ta-.
(a)    –na- katika kuonesha wakati uliopo
Mfano, Wanatembea.
             Anakula.
(b)   –li- hii huonesha wakati uliopita
Mfano, Watoto walicheza mpira.
             Walimu walifundisha.
     (c) -ta-  hii huonesha wakati ujao katika tungo.
 Mfano, Mwalimu atafundisha kesho.
              Rehema atarudi wiki ijayo.
Kategoria ya idadi. Hii ni kategora ya sarufi mapokeo ambayo huonesha idadi katika tungo zinazohusu umoja na wingi. Mara nyingi huonekana katika nomino na aina zingine za maneno  kama vile vitenzi na vivumishi.
Mfano.
(a)   Mtoto anakimbia. (umoja)
     Watoto wanakimbia . (wingi)
(b)   Msichana mzuri . (umoja)
     Wasichana wazuri. (wingi)
Kwa kurejerea mifano hii viambishi  m-  na  wa-  kwa pamoja ni kategoria za idadi.
Kategoria ya hali. Hii ni kategoria ya kisarufi mapokeo ambayo huelezea  utendekaji wa lile tendo ambalo lawezakuwa katika hali timilifu yenye kiambishi  -me- au hali ya mazoea yenye kiambishi hu-
Mfano; -me- katika hali  timilifu
(a)    Mwanaidi ametoroka nyumbani.
(b)   Mwalimu amefundisha kiswahili.
(c)    Juma amekimbia kichakani.
Mfano;  hu- katika hali ya mazoea
(a)    Mutta hufundisha Kiswahili.
(b)   Tababa hutembea harakaharaka.
Kategoria ya jinsia; hii ni aina ya kategoria ya kisarufi mapokeo ambayo hubainisha maumbile katika tungo.  Zipo jinsia za aina mbili.
(a)    Jinsia ya kibaiolojia
(b)   Jinsia ya kisarufi
(a)    Jinsia ya kibaiolojia; hii ni aina ya jinsia  inayohusu maumbile ya mtu .Aina hii  husawiriwa na lugha. Aidha katika lugha ya Kiingereza maneno kama Patron, He, Boy na Headmaster hudokeza jinsia ya kiume ilhali yale ya Matron, She, Girl na Headmistress hudokeza jinsi ya kike.

(b)   Jinsia ya kisarufi; udhihilishwa na maneno ya augha kuwekwa kwenye makundi bila kuzingatia kigezo cha kibaiolojia. Hata hivyo, baadhi ya nomino katika lugha ya Kiswahili mfano; msichana, mvulana, bibi, Baba , mama, kaka, dada na babu hudokeza jinsia.
Kategoria ya dhamira. Mtei (2008 uk.140); anaeleza kategoria ya dhamira na kuanza na fasili ya dhamira kuwa  ni  kipengere cha kisarufi na kimaana ambacho huonesha lengo/ maana/ mwelekeo inayoiburiwa na vitenzi mbalimbali katika sentensi. Baada ya fasili hii amabainisha aina za dhamira kama ifuatavyo;
(a)    Dhamira elezi/ arifu;  hii hutumiwa kueleza ukweli wa mambo jinsi ulivyo vilevile hutoa taarifa kuhusu jambo.
Mfano, (i) Mzozo huu umetatuliwa.
            (ii) Mwizi yule alikamatwa.
(b)   Dhamira amrishi; anaieleza kuwa nidhamira ambayo hutumiwa kuonesha amri, ombi/ kutahadharisha.
Mfano, (i) Simama juu.
            (ii) Lete hilo jembe.
© Dhamira tegemezi; hii hutumiwa kuonesha hali ya kutokuwa na hakika au uwezekano wa mambo au kutokea kwa matukio .
            Mfano, (i) kutokuwa na hakika.
      (a) Labda hakupata taarifa zako.
                              (b) Ikiwezekana nitakuja nae.
                       (ii) kutegemea kwa matukio.
            Mfano,  (a) Mwalimu angenipa mtihani wangu ningeweza kufanya masahihisho.                                                                      
              (b)  Shule zikiongezeka watoto wengi watapata elimu.
      (iii) uwezekano wa jambo.
Mfano,  (a) Mvua ingenyesha asubuhi tu.
                          (b) uzembe wake ungedhibitiwa mapema.
Kategoria ya kauli; katika kufafanua dhana hii Matinde (2012:190-205) anaeleza dhana ya kauli kuwa, ni kategoria ya kisarufi ambayo uamilifu wake umekitwa katika  kitenzi. Pia amezibainisha kauli mbalimbali zinazojitokeza katika lugha ya Kiswahili kama ifuatavyo;
I.                   Kauli ya kutendwa; hii ni kauli  ambayo hubainisha kuwa kiima ni mtendewa au mtendwa.
Mfano,  (i) Uwanja umefyekwa.
              (ii) Nyumba imechomwa.
II.                Kauli tendi; hii ni kauli ambayo hubainisha kuwa kiima ni mtenda. Kauli hii  huonyesha kuwa nomino iliyopo kwenye kiima ndiyo; ilitenda, itatenda, au inatenda kitendo husika katika tungo.
   Mfano. (i) Mwajuma alipanda maboga.
               (ii) Mwalimu anafundisha.
       III. Kauli ya kutendeka; hii haioneshi uhusiano ulio wazi baina ya kiima na yambwa. Hata                                                  hivyo, kiima hupata athari kutokana na kitendo husika. Katika kauli hii alomofu zinazoonesha kauli hii ni {-ik-}, {-ek-}, {-lik-}, {-lek-}, {-ikan-} na {-eken-}.
Mfano, (i) Nyumba inaanguka.
            (ii) Kiti kimevunjika.                                                                                         
           (iii) Fanyika
          (iv) Vukika
          (v) Tosheka
     (vii) Ngoma hiyo haikututeka.
V.                Kauli ya kutendewa; hii hujumuisha vitenzi vinavyotokana na kauli ya kutendea kuongezewa viambishi. Alomofu zake ni {–w-}, {-liw-}, {-iw-} au {-ew-}
Mfano, (i) Pigwa
                  (ii) Cholewa  
                  (iii) Imbiwa
VI.             Kauli ya kutendeka; hii ni kauli ambayo huonesha jinsi jambo linavyotendeka. Alomofu zinazobainishwa katika kauli hii ni {-ek-}, {-ik-}, {-lik-}
  {-elek-}, {-ikan-}, na {-iken-}.
Mfano; (i) pigika
           (ii) chezeka
          (iii) Someka
VII.          Kauli ya kutendua; kauli hii hudhihirishwa na kinyume cha utenduzi. Alomofu za kauli hii ni. {-u-}, {-a-}, {-i}, {-e-}.
Mfano: (i) Fungua
            (Ii) Umbua
            (Iii) Chomoa

VIII.       Kauli ya kutendana; hii ni kauli ambayo hubainisha  uhusiano fulani kati ya kiima na yambwa. Alomofu za kauli hii ni {-an-}
  Mfano.  (i) Sukana
                                   (ii) Chekana
                                    (iii) Somana
IX.             Kauli ya kutendesha; hii ni kauli ambayo hubainisha dhana ya usababisho kati ya kiima na yambwa. Alomofu zinazojitokeza katika kauli hii ni: {-esh-}, {-lesh-},            {-lish}, {-ez-}, {-iz-} ambazo hutegemea vitenzi husika katika tungo.
Mfano; (i) Ogesha
            (ii) Pigisha
           (iii) Chezesha
Kategoria ya uhusika; Matinde (2012:207), ameeleza uhusika kuwa ni kategoria ya kisarufi ambayo huonyesha uhusiano wa viambajengo katika tungo. Aidha huonyesha uamilifu wa kila kiambajengo katika tungo na athari ya kila kiambajengo hicho kwa viambajengo vingine. Uhusika huu huweza kugawanyika katika aina sita kama ifuatavyo;
(i)                 Uhusika wa kiima; huu hubainisha kuwa nomino, au kiwakilishi chake huchukua nafasi ya kiima.
   
Mfano: (a) Daktari alimkaribisha mgonjwa.
                          (b) Musa amejengewa nyumba .
  (ii)      Uhusika tendea; uhusika huu huonyesha kuwa nomino au kiwakilishi chake                     kinathirika kutokana na tendo fulani.
                        Mfano: (a) Mwiba ulimchoma Jeska.
                                (b) Yeye alifukuzwa na mwalimu.
(iii) Uhusika ala; huu huonesha kitu ambacho hakina hisia kilichotumika katika         kutekeleza kitendo au jambo fulani. Kifaa hiki hutumika kusababisha utokeaji wa tendo au hali ambayo inadokezwa na kitenzi.
Mfano: (a) Alivunja mlango kwa nyundo.
            (b) Alimkata kwa panga.
(iv) Uhusika yambwa; huu huonyesha kuwa nomino au kiwakilishi chake kimechukua nafasi ya yambwa katika tungo.
            Mfano: (a) Jumanne alinunuliwa baisikeli.
            (a)  Mfano: Mwanafunzi aliyefauru vizuri awazawdiwa daftari.
(v) Uhusika mahali; huu hubainisha mahali au mwelekeo wa kieneo wa hali au tendo ambalo  linadokezwa na kitenzi.
            Mfano: (a) Mbwa yuko nyuma ya kabati.
                           (b) Ameweka jagi chini ya meza.
(vi) Uhusika  mtendwa au mtendewa; huu hudhihirisha kiumbe chenye hisia ambacho kinathirika na hali au tendo linalodokezwa na kitenzi.
Mfano: (a) Mtoto aliangushwa naa mbuzi wake.
               (b) Yule msichana amechomwa na mwiba.
Kategoria ya ngeli; Wahiga (1999:40), analeza maana ya ngeli kuwa ni jamii ya nomino zenye kuleta mabadiliko ya aina moja ya viambishi vya maneno katika umbo la umoja na wingi. Masebo na wenzake (2003) wanaeleza kuwa, huu ni mtazamo mkongwe zaidi uliofuatwa na wanasarufi mapokeo ambao miangoni mwao alikuwa ni Meinholf baadaye akafuatwa na Broomfeld (1931) na Ashitoni (1944) ambao waliziainisha nomino kulingana na viambishi awali vya nomino. Nomino zote zilizokuwa na viambishi vinavyofanana ziliwekwa katika kundi moja na kufanya ngeli moja.
Mfano ni katika jedwali lifuatalo;

Ngeli
Viambishi awali vipatanishi
Mifano
1
A-WA
A-    Umoja
WA- wingi
Mtoto anakuja - watoto wanakuja
Mwalimu ameondoka - walimu wameondoka
2
U-I
U- umoja
I-wingi
Mmea umenyauka - mimea imenyauka
Mkungu umenunuliwa - mikungu imenunuliwa
3
LI-YA
LI-Umoja
YA- wingi
Yai limepasuka - mayai yamepasuka
Embe limeoza - maembe yameoza
4
KI-VI
KI- Umoja
VI- Wingi
Kiti kimevunjika - viti vimevunjika
Kikombe kimekatika - vikombe vimekatika
5
I-ZI
I-umoja
ZI- wingi
Nyanya imechumwa - nyanya zimechumwa
Soda imeuzwa - soda zimeuzwa
6
U-ZI
U- umoja
ZI-wingi
Ufunguo umepotea - funguo zimepotea.
Uzi umenunuliwa - nyuzi zimenunuliwa.
7
U-YA
U- Umoja
YA- wingi
Ugonjwa umeenea - magonjwa yameenea
Uasi umeisha - maasi yameisha
8
KU
KU- Umoja
Kusuka kunachosha
Kuigiza kunaburudisha
9
PA-MU-KU
PA-umoja
MU-Umoja
KU- umoja
PA- Mahali hapa pananuka
MU- Mahali humu munamaji
KU- Mahali kule kuna giza.
Kwa hiyo, licha ya wanasarufi mapokeo kutumia lugha ya kilatini kama kigezo cha kupima ubora wa lugha kuwa ni makosa kwa sababu ya kuwa kila lugha ina mtindo wa kipekee wa kuunda tungo zake, lakini faida kubwa inayojitokeza kwa wanasarufi mapokeo ni kuwa waliweza kuanzisha kategoria mbalimbali za kisarufi ambazo zinatumika mpaka sasa katika uga wa sarufi.





  MAREJELEO
Masebo na wenzake, (2002).  Kiswahili Kidato cha 3 na 4. Nyambari Nyangwine Publishers:
                          Dar es Salaam.
Massamba na wenzake, (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA). TUKI:
                          Dar es Salaam.
Matei, A. K. (2008). Darubini ya Sarufi. Phoenix Publishers: Nairobi.
Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha; Isimu na Nadharia. Serengeti Educational Publishers
            (T) Limited: Mwanza.    
Philipo, Z. (2013). Sintaksia ya Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dodoma: Dodoma.
Waihiga, G. (1999). Sarufi Fafanuzi ya Kiswahili. Longhorn Publishers: Nairobi.
www.chombozi.blogspot.com. (Ilitembelewa tarehe 23/12/2014 saa 04:30 usiku.)
www.englishclub.com. (Ilitembelewa tarehe 23/12/2014 saa 05:45 usiku.)
www.out.ac.tz. (Ilitembelewa tarehe 23/12/2014 saa 05:50 usiku.)
www.thefreedictionary.com. (Ilitembelewa tarehe 24/12/2014 saa 07:01 usiku.)

Maoni 28 :

  1. Inapendeza sana na inasaidia kuongeza ufahamu.HONGERA

    JibuFuta
  2. swali.jadili ni kwa nini hamna lugha bora wala duni?

    JibuFuta
    Majibu
    1. Kilonzi Enoch, ni kweli hakuna lugha bora wala duni kwasababu kuu mbili: kwanza, kila lugha ina sifa ya kujitosheleza kimatumizi. Wazungumzaji wa (tuseme) lugha ya kimasai hukamilisha mawasiliano yao bila msaada wa lugha "bora" yoyote. Pili,Lugha yoyote huweza kuwa na hadhi kubwa kutegemea hali ya kiuchumi, kisiasa,na kiteknolojia. Kwa mfano lugha ya Kiingereza INA hadhi kubwa kutokana na sababu za kihistoria za wazungumzaji wake - wazawa.

      Nb: lugha yenye hadhi kubwa ni ile ambayo imekua kimatumizi eneo kubwa la kijiografia, huwa na kamusi, hutumika maeneo mengi rasmi, huwa na sarufi ambayo hufundishwa shuleni, nk lakini haya yote ni mambo ya ziada sana. Jambo la msingi katika lugha ni kukamilisha mawasiliano katika jamii fulani sifa ambayo lugha yoyote inayo.

      Futa
  3. Tafadhali naomba outline :Kwa kutumia nadharia ya sarufi mapokeo, eleza mambo makuu matatu wanayosisitiza kuhusu sintaksia ya lugha na Kisha toa maoni yako kwa kuzingatia wakati huo wa Enzi za mapokeo na wakati wawakati wa sasa

    JibuFuta
  4. Nisaidie aina za maneno kwa mtazamo wa kimuundo

    JibuFuta
  5. Swali:
    1. Jadili Kategoria za kisarufi
    a). Kimuundo
    b). Toa ushahidi wa kuwepo kwa kategoria hizo katika lugha

    JibuFuta
  6. Kazi nzuri nimepata maarifa mapya. Tunaomba ungetuma na ushahidi wa kuwepo Kwa kategoria za kileksika

    JibuFuta
  7. Jadili ubora wa sarufi elekezi

    JibuFuta
  8. Naomba utuelezee kategoria za kileksika kwa mifano

    JibuFuta
  9. naomb ufafanuzi juu ya Kaategoria ya jenda/ jinsia ma aina za kategoria hiyo

    JibuFuta
  10. Udhaifu wa makabala wa kimapokeo niupi?

    JibuFuta
  11. Umechambua vizurii kategoria za kisntksia kwa mkbla wa kimapokeo

    JibuFuta
  12. Umechambua vizurii kategoria za kisntksia kwa mkbla wa kimapokeo

    JibuFuta
  13. Dhihirisha mitazamo mitatu ya kikategoria kwa kina kisha toa maoni juu ya mtazamo faafu. Naomba nisaidie ili swali

    JibuFuta
  14. udhaifu wa wanasarufi mapokeo ndio chanzo cha sarufi za kisasa.jadili

    JibuFuta
  15. Shukrani Sana hakika nimeongeza nashida mapya

    JibuFuta
  16. Kazi nzuri hongera sana

    JibuFuta
  17. Hongera. nina swali
    Zikague sentensi Kisha uyajibu maswali yanayofuata.
    1.juma amelala
    2.juma alimpiga hamisi
    3.juma alimpikia hamisi chakula
    4.wanafunzi humchaguaHamisi kiranja wao kila mwaka.
    Maswali
    1.kwa kila mojawapo ya sentensi hizo. Yaainishe maneno yaliyotumiwa katika Kategoria za kisarufi.
    2.uainishe muundo WA kila sentensi ukizingatia uamili WA maneno uliotumika.
    3.kwa kila sentensi chora kielelezo matawi.

    JibuFuta
  18. asante sana nimeweza kuongeza ufahamu.

    JibuFuta
  19. Hongera umefanya kazi nzuri sana

    JibuFuta
  20. Nimeelewa Sana hongera

    JibuFuta
  21. Ahsante sana nimepanua wigo wa ufahamu juu ya sintaksia

    JibuFuta
  22. Nakala ipo vizuri hivyo ni vyema kwa mtunzi kuiendeleza haiba yake ya utunzi hata katika mawanda mengine ya kisarufi Kama vile wanamuundo.

    JibuFuta