Jumapili, 1 Novemba 2015
Alhamisi, 25 Juni 2015
IDADI YA WAGOMBEA URAISI YAONGEZEKA
IDADI ya wagombea wanaochukua fomu kwa ajili ya kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana walifikia 39 baada ya mwanachama wake, Ritha Ngowi kuchukua fomu.
Ngowi, mkazi wa Dar es Salaam, anakuwa mwanamke wa tano kuchukua fomu, ambapo waliochukua fomu wa awali ni Balozi Amina Salum Ally, Waziri wa Katiba na Sheria Dk Asha-Rose Migiro, Dk Mwele Malecela na Monica Mbega.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema yeye ni msomi ambaye ana shahada ya Maendeleo ya Jamii na pia amepitia kozi mbalimbali katika ngazi za diploma na cheti. Alisema vipaumbele vyake vitakuwa ni kwenye sekta ya elimu na uchumi.
“Nimeguswa sana na kuamua kugombea nafasi ya Urais lengo langu kubwa ni kutaka kuboresha elimu na Uchumi” alisema.
Alisema iwapo atachaguliwa kuwa Rais atahakikisha kila Mtanzania anapata elimu ya msingi na asiwepo Mtanzania asiye na uwezo wa kupata kipato na atahakikisha Watanzania wanawezeshwa ili kuwe na uzalishaji.
Kwa upande wa uchumi alisema atamairisha vivuko kwa ajili ya kupunguza foleni, na wakulima watapatiwa pembejeo na mazao yao yatatafutiwa masoko.
Hata wafanyabiashara kazi zao katika mazingira mazuri na wafanyakazi wa serikali watapata mishahara mizuri itakayowezesha wananchi kuishi maisha yenye viwango. Alisema atarekebisha mishahara kuanzia ngazi ya chini.
“Unaweza kuona mtu anapokea mshahara wa Sh 350,000 hadi 450,000 anapanga nyumba na analipa ada, maslahi yao lazima yarekebishwe,” alisema.
Alipohojiwa kama ana sifa 13 za mgombea wa CCM anavyo alisema anazo sifa hizo zote ndio maana amejitokeza. Pia alipohojiwa atatanuaje tatizo la rushwa iwapo ataingia madarakani, alisema ili kuondoa tatizo la rushwa jambo la kwanza ni kudhibiti vyanzo hivyo.
Alisema kutakuwepo na mikakati ili fedha zote zinazokusanywa zifike kwenye vyanzo husika na huduma zifike mahali panapostahili.
Katika historia yake alisema amewahi kufanya kazi Shirika la Uchumi na Maendeleo ya Wanawake Tanzania (Suwata) pia aliwahi kufanya kazi Chama cha Wasioona Tanzania, pia mmiliki wa shule ya sekondari ya Jostihego iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Mawaziri 2 warudisha fomu Wakati huo huo, mawaziri wawili wanaowania kuteuliwa na CCM, kuwa wagombea wa nafasi ya Urais jana walirudisha fomu. Waliorudisha fomu ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri wa Kilimo na Ushirika Steven Wassira.
Balozi Karume Mgombea mwingine, Balozi Ally Karume alirejesha fomu yake saa 10.35 jioni. Alichukua fomu hiyo Juni 4, mwaka huu na kwenda kutafuta wadhamini katika mikoa mbalimbali ya Bara na Visiwani, mwenyewe akisema amepata wadhamini wa kutosha na wengine wa ziada.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu amesema CCM ni chama pekee nchini ambacho kimefanikiwa na kinaendelea kupanua wigo wa demokrasia.
Nyalandu ni miongoni mwa wanachama wa chama hicho nchini waliotia nia ya kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi ujao, aliyasema hayo jana wakati anazungumza na viongozi na wanachama wa CCM wilayani Masasi waliojitokeza kumdhamini.
Alisema hakuna tunu bora nchini zaidi ya kuendeleza umoja, amani na mshikamano uliopo hivi sasa ndani ya chama hicho huku akitoa mwito kwa wagombea wenzake ndani ya chama kuacha kukitia madoa chama na hata wao wenyewe, kwani kwa sasa CCM inahitaji umoja.
Alisema wana CCM nchini waondoe tofauti zao kwa kuwa ndiyo silaha pekee itakayoirudisha madarakani ambapo pia aliwaasa watanzania kupinga vitendo vyote vya kibaguzi, udini, ukabila na hata tofauti za rangi na kwamba endapo CCM kitampa ridhaa ya kuwa mgombea wa urais atahakikisha vitendo hivyo vinabaki kuwa historia.
Kwa mujibu wa Nyalandu, amekuwa CCM kwa muda mrefu sasa na kwamba kwa sasa Mungu ameruhusu kizazi kingine kipate fursa ya kuongoza nchi lengo likiwa ni kujenga uchumi imara kwa kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo gesi, mafuta, milima pamoja na hifadhi za Taifa.
Jisajili Nasi
Jumamosi, 6 Juni 2015
TAFSIRI YA KISAYANSI NA TEKNOLOJIA (TAFSIRI YA KIUFUNDI)
Kazi ya tafsiri haifanywi kiholela bali
huzingatia baadhi ya hatua ili kufikiwa kiufanisi. Kwan kumrejelea Mwansoko
(2006), anabainisha hatua zifuatazo:
Kwanza, mfasiri akabiliwapo na matini ya
sayansi na teknolojia kwanza aisome kwa makini ili kuelewa maudhui yake. Lengo
ni kufanya matini lengwa iakisi matini chanzi kiujumbe, zaidi ni kupigia
mistari katika maneno magumu ili kuweza kuyatafutia maana katika vyanzo
mbalimbali kama vile, kamusi ili kufanikisha zoezi la tafsiri.
Pili, ni kutathimini ubora wake. Mfasiri anapaswa kuchunguza ubora wa matini
chanzi, ili kuangalia kiwango chake cha urasimi yaani umaalumu kwa mfano;
istilahi zilizotumika ni za kisayansi, mifano iliyotolewa inahalisika
kisayansi, au mambo yanayoongelewa ni ya kisayansi. Jumla ya mambo haya
yanatakiwa kuzingatiwa na mfasiri kwani yanathibitisha uhai wa matini ya kiufundi.
Tatu, baada ya kuchambua matini yako
ifasiri hasa kwa mkabala wa sentensi kwa sentensi. Mkabala huu unasisitizwa
kwani unaeleweka zaidi kuliko wa neno kwa neno ambao kimsingi huweza kutuletea
maana tenge katika tafsiri.
Nne, iweke tafsiri yako katika umbo
linalotakiwa na mteja wako. Mfano; kama unafasiri kwa ajili ya shirika fulani
la uchapishaji fuata mtindo wa machapisho ya shirika hilo kwa kuzingatia
machapisho ya awali, na kama unafasiri gazeti au jarida fuata mtindo wa uandishi
wake.
Baada ya kuangalia hatua za kufuata
katika kufasiri matini za kisayansi na teknolojia, ufuatao ni mtindo wa lugha
ambao mara nyingi hutumika katika kufasiri matini hizo:
Mwansoko (1994) na (2006), ameonesha
mtindo wa lugha unaotumika katika tafsiri ya kiufundi (sayansi na teknolojia).
Kwa kawida, lugha inayotumika katika tafsiri ya kiufundi huwa na lengo la
kueleza usahihi na ukweli wa mambo yanayojadiliwa. Hivyo nia ya mwandishi hapo
sio kusisimua au kuibua hisia au maono ya wale wanaomsoma au kumsikiliza, bali
ni kutoa taarifa tu kama ilivyo. Lugha inayotumika katika tafsiri ya kiufundi
kwa kawaida haina mhemko au jazba, ni ya msimamo wa katikati. Kutokana na sifa
hizo tunapata mambo yafuatayo:
Hutumia sana kauli za kutendwa. Kauli
hizi hutumika sana hata kama mwandishi ameandika kazi yake peke yake. Hii
hutumika ili kuondoa dhana ya umilikishi katika uga wa taaluma.
Mfano;
Masuala yaliyopendekezwa,
Jambo lililojadiliwa,
Imedhihirishwa,
Inapendekezwa,
Imekubaliwa n.k.
Jambo jingine ni matumizi makubwa ya
vitenzi vya kidhahania. Vitenzi hivyo vya kidhahania ni vile ambavyo havioneshi
au kubainisha waziwazi nafsi ya mtenda/mtendwa ama kubainisha mhusika. Matini
za sayansi na teknolijia hazioneshi umiliki kama zifanyavyo za taaluma zingine
kama fasihi.
Mfano;
Kutembelea vikundi mbalimbali vya
sanaa,
Kusoma tafsiri,
Ukimwi unaua chukua tahadhari.
Vilevile, ina matumizi makubwa ya nafsi
ya kwanza wingi mahali pa nafsi ya kwanza umoja. Mtindo wa lugha katika tafsiri
matini za kiufundi hukwepa matumizi ya nafsi ya kwanza umoja na badala yake
hutumia nafsi ya pili wingi ikiwa na lengo la kufanya watumiaji wa matini ile
kuamini kuwa imefanywa na watu wengi.
Mfano; Katika
sura inayofuata tutachambua kwa undani zaidi mtindo wa kirasimi...
Mwansoko (1994:26)
japo kitabu hichi kakiandika mwenyewe lakini katumia wingi.
Tunakubaliana na mawazo ya….
Tunazungumzia….
Kadhalika,
hutumia sana kauli zisizoonyesha nafsi ya mtendaji. Hii inajidhihirisha pale
ambapo mwandishi anakua kama amejitoa katika matini Fulani na kuonekana si
muhusika kwa kuweka baadhi ya vipashio ambavyo havioneshi nafsi dhahiri. Hivyo
tafsiri ya matini za kiufundi huwa na sifa hiyo.
Mfano,
Imeafikiwa kuwa
Imeadhimiwa kwamba
Ilipendekezwa yafuatayo
Inatazamiwa kwepo na…
Baada ya kuangalia mtindo wa lugha
unaotumika katika matini za sayansi na teknolojia, sasa tuangalie sifa bainifu/upekee
wa matini za sayansi na teknolojia kama ifuatavyo:
Kwanza, hazijigezi na utamaduni wowote.
Hii ni kwa sababu matini hizi hutarajiwa kutumiwa na watu wote/ulimwengu mzima
na hii ndio maana mara nyingi katika matini za kisayansi majina au istilahi
huandikwa kama yalivyo bila kujali athari zake/ukali wa maneno hayo kwa
utamaduni wa jamii fulani. Kwa mfano sehemu za mwili wa bianadamu mathalani
uke, uume, puru, korodani nakadhalika huandikwa bayana bila kujali nani
anapelekewa matini hizo, ana umri gani, heshima gani, au yuko katika muktadha
upi. Mfano mzuri tunaweza kurejelea katika vitabu vya sayansi shule za msingi
(darasa la sita) ambapo kuna michoro inayobainisha sehemu mbalimbali za mwili
wa mwanadamu. Halikadhalika katika zana mbalimbali za kiufundi mfano katika
karakana kuna kifaa kinachojulikana kama Mult-purpose
spanner ambacho kwa Kiswahili kimetafsiriwa kama spana malaya. Hivyo kwa
kiasi fulani kulingana na utamaduni wa waswahili kuna ugumu fulani katika kuzitaja
au kuzirejelea zana au vifaa tajwa hapo juu, na wengine huona kuwa ni matusi.
Tafsiri za matini ya sayansi na
teknolojia ina matumizi makubwa ya istilahi. Msokile, (1993) anaeleza kuwa,
istilahi ni neno litumikalo kwa ufupi wa maneno mengi ya kiufundi kufuatana na
ujuzi ama elimu maalumu. Kwa mfano, istilahi za fasihi, istilahi za kemia na
jiografia. Katika uga wa sayansi kuna istilahi mbalimbali kama ifuatavyo:
Istilahi za Hisabati ni sphere, triangle, pai na algebra.
Istilahi za Baiolojia ni genetic, photosynthesis, nutrition na excretion.
Istilahi za Kemia ni calcium, element, potassium na carbonate.
Istilahi za Fizikia ni electric, current, ampere na voltage.
Katika istilahi, huwa kuna ugumu katika kupata au kutambua maana za
istilahi mpya kwa mfasiri hasa zile ambazo hazifungamani sana na muktadha na
hutokea mara moja tu katika matini. Mkabala ulio bora zaidi kwa matini ya
kiufundi yenye istilahi nyingi za uvulivuli, ni kupigia mistari istilahi
zinazoonekana kuwa ni za msingi wakati usomapo matini chanzi kwa mara ya kwanza
na kisha tafuta maana zake kwenye kamusi. Istilahi hizo zinaweza kuwa na maana
zaidi ya moja katika Nyanja moja ileile.
Wakati
mwingine yawezekana ukakosa kabisa visawe vya istilahi za lugha chanzi katika
lugha lengwa yako. Hali hii inapotokea mfasiri hulazimika kuunda istilahi zake
mwenyewe kwa kutumia mbinu ambazo hutumiwa na lugha zote kuzalisha maneno
mapya. Mbinu hizo ni pamoja na kutumia lugha lengwa yenyewe kwa minyumbuliko,
miambatano, miungano, upanuaji wa maana za maneno yaliyopo na
uhulutishaji. Vilevile, mbinu ya kukopa
kutoka lugha nyinginezo, lahaja, istilahi za kimataifa pamoja na tafsiri sisi.
Upekee wa mwingine wa tafsiri za
kiufundi au za kisayansi na teknolojia, kwa kawaida huwa katika umbo la ripoti
ya kiufundi, lakini yawezekana pia ikajumuisha vitabu vya rejea, maelekezo au
notisi zinazoandikwa kwa kufuata mtindo wa maandiko ya kitaaluma. Hivyo upekee
huu ndio unaoitofautisha matini ya kisayansi na matini zingine ambazo si za
kisayansi. Na sifa hii ndiyo huweza kuitofautisha na matini nyingine kama za
kifasihi, kisheria, kidini na zingine ambazo zinakuwa katika umbo la sentensi
au katika aya ndefu, zisizokuwa katika mwonekano wa chati, grafu, orodha
vielelezo, picha kama ilivyo katika ripoti. Hili limeshadadiwa katika ukurasa
unaofuata. Pia, katika hoja ya kujumuisha vitabu vya rejea, kama kamusi, orodha
ya istilahi na marejeo mengine ni muhimu katika tafsiri ya kiufundi kwa sababu
kuna baadhi ya istilahi zinakuwa na maana zaidi ya moja. Kwa hiyo ni vyema
kurejelea katika marejeo ili kupata maana mahususi ya istilahi inayoendana na muktadha
husika. Kwa mfano; rejeleo lililoambatanishwa katika ukurasa unaofuata. Lakini
pia mara nyingine, matini hizi za kiufundi huweza kuwa tu katika mfumo wa notisi
au maelekezo ya kitaaluma kama vile, vitabu vya Baiolojia, Kemia, Jografia na
taaluma zingine za kisayansi.
Upekee mwingine ni kuwa, tafsiri ya
matini za kisayansi na teknolojia hutumia rejesta mbalimbali pamoja na
kuonekana imeandikwa vibaya. Rejesta ni mtindo wa lugha inayotumika mahali
penye shughuli maalumu inayotumiwa na kundi maalumu la wanajamii. Matumizi ya
rejesta nyingi katika tafsiri hii hutokana na tafsiri hii kuwa na mada nyingi
tofauti na tafsiri nyingine. Mfano katika vitabu vingi vya sayansi huwa na mada
nyingi zilizochambuliwa tofauti na vitabu vya sanaa kama fasihi. Vilevile
rejesta nyingi hutokana na mazoea ya watumiaji kama vile, mafundi magari,
mafundi baiskeli, watu wa uhandisi na wengine. Kwa mfano fundi baiskeli hutumia
rejesta kama vile;
Siti kava – kumaanisha
sehemu anayokaa anayeendesha baiskeli
Stelingi – kumaanisha
usukani
Breki – vifaa vya
kufunga ili kupunguza mwendo
Sahanipeda – kifaa kama
sahani ambacho hushika mnyororo
Medigadi – kifaa cha
kukinga tope kinachopatikana katika gurudumu
Tairi – gurudumu
breki filiwili kiti stelingi
spoku
Tairi (gurudumu)
gia padeli
Rejesta na maneno yaliyofasiriwa hapo
juu ni ya kisayansi na mwonekano wake na namna yanavyosikika katika lugha ya
Kiswahili yanaonekana kutokuwa vizuri (hayavutii). Siyo hayo tu, pia hata
katika simu tunazozitumia tafsiri ya maneno kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili
zinaonekana kuwa na ukakasi huo huo uliojitokeza hapo juu. Kwa mfano;
Setting – mipangilio
Phone book – majina
Profile – mifumo
Alarm – kengele
Torch
– taa
Images – picha
Sms
– ujumbe
Hiyo ni kwa mujibu wa shirika la simu
linaloitwa Nokia.
Kwa
kuhitimisha tunaweza kusema kuwa, tafsiri ya sayansi na teknolojia ina
upekee sana japo inakabiriwa na changamoto mbalimbali kama vile, ugumu wa
upatikanaji wa istilahi za kisayansi na ugumu wa kupata maana za maneno au
istilahi hizo za kisayansi na teknolojia. Hivyo changamoto hizo zinaleta shida
katika tafsiri ya matini za sayansi na teknolojia.
MWALIMU MWANAFUNZI (USHAIRI)
NA
RICHARD, KASHINJE 0764711129
rkashinje@gmail.com
MWALIMU
MWANAFUNZI
1 Mwalimu uwe makini, makini kumakinika
Mwalimu
si masikini, akilize kulabuka.
Walimu
sikilizeni, yamoyo yalotukuka
Mwalimu
ni mwanafunzi, kusoma hana kikomo.
2 Siku uwapo kazini, kusoma huna kikomo
Hata
kama nimezani, kitabu hakina komo
Pata
yawanazuoni, mapya kwako yaliyomo
Mwalimu
ni mwanafunzi, kusoma hana kikomo
3 Usishike mazoea, kusoma moja pekee
Kusema
umebobea, hakika si wapekee
Kazi
yako watachukua, waliosoma pekee
Mwalimu
ni mwanafunzi, kusoma hana kikomo
4 Usipokuwa msomi, tena wakusoma sana
Wanafunzi
hawakusomi, kwako ni aibu sana
Hawatakupenda
msomi, na hiyo fedheha sana
Mwalimu
ni mwanafunzi, kusoma hana kikomo
5 Kumbuka ile kauli, ambayo kwetu nirai
Mwalimu
kuwa mkali, wanafunzi kuzirai
Kwako
murua kauli, kwao somo wafurai
Mwalimu
ni mwanafunzi, kusoma hana kikomo
6 Siku zimebadilika, yakupasa utambue
Wanafunzi
huzunguka, ukweli wautambue
Yakupasa
kumakinika, wasomi wasiumbue
Mwalimu
ni mwanafunzi, kusoma hana kikomo.
7 Msomi tulikuamini, tuakukabidhi kazi
Kwakuwa
niutamaduni, nzuri ufanyapo kazi
Pia
tuanatatumaini, kazi iota mizizi
Mwalimu
ni mwanafunzi, kusoma hana kikomo
8 Kusoma hana kikomo, mwalimu ni
mwanafunzi
Mwanafunzi
hana komo, kusoma ni mwanafunzi
Haya
ndani yawe yamo, kazi ni uwanafunzi
Mwalimu
ni mwanafunzi, kusoma hana kikomo
Mashairi ya kiswahili
USHAIRI
WA KISWAHILI
HAKI
1 Maisha haya jamani, kweli niipatashika
Maisha
kama majani, kweli yanapukutika
Maisha
yalo gizani, leo yaanasikika
Haki
yamtu jamani, hakika nipatashika.
2 Tuliishi kwaamani, tena kwakujiamini
Haki
zetu mikononi, wote tulizitieni
Lakini
wetu karani, leo twamzikeni
Haki
ya mtu jamani, hakika nipatashika.
3 Kila mnyonge nyumbani, wote
walifurahia
Swahibu
kwake moyoni, kwake alipigania
Amani
kwetu moyoni, wote tulisherekea
Haki
ya mtu jamani, hakika nipatashika.
4 Kichwa chake chahekima, busara zimesimama
Kelo za watu mapema, tayari kuzitazama
Waume
na kinamama, haki hawakulalama
Haki
ya mtu jamani, hakika nipatashika.
5 Tuliishi kwa matao, busara yake karani
Karani
wetu mtwao, sote twaweka kirini
Twakukumbuka
wanao, leo hii korokoroni
Haki
ya mtu jamani, hakika nipatashika.
6 Mungu ulo mbinguni, sikia hiki kilio
Mjalie
wetu karani, korokoroni kilio
Wote
tunamdhamini, twomba tena kwakilio
Haki
ya mtu jamani, hakika nipatashika.
NA
RICHARD, KASHINJE 0764711129
rkashinje@gmail.com
MIIKO YA KABILA LA WAKEREWE
Falsafa nidhana nyeti sana katika
maissha na utamaduni wa wabantu waishio
katika bara la Afrika. Katika kujadili swali hili tutaanza kujadili dhana za
Falsafa jinsi ilivyoelezwa na wataalamu mbalimbali, tutaleleza maana ya miiko
jinsi ilivyoelezwa na vyanzo mbalimbali, tutaeleza historia fupi ya wilaya ya
Ukerewe, tutaeleza kiini cha swali letu ambapo tutakeleza miiko mbalimbali
ambayo inapatikana katika kabila la Wakerewe na hatimaye tutahitimisha kwa
kutoa tathimini ya miiko hiyo kwa sasa jinsi inavyochukuliwa. Tuanze kwa
kuziangalia maana mbalimbali za Falsafa jinsi ilivyojadiliwa na wataalamu
mbalimbali kama ifuatavyo;
http://sw.wikipedia.org/wiki/Falsafa Falsafa ni jaribio la kuelewa
na kueleza ulimwengu
kwa kutumia akili inayofuata njia ya mantiki kwa kuchunguza mambo kama kuweko
na kutokuweko, ukweli, ujuzi,
uzuri, mema na mabaya, lugha,
haki na mengine yoyote.
http://pengotz.blogspot.com/2007/12/falsafa-ya-elimu-tanzania.html wanaeleza kuwa,
falsafa ni taaluma inayojishughulisha na kutafuta ukweli wa jambo kwa njia ya
kutafakar.
Kwa ujumla tunaweza kuseama kuwa, Falsafa ni tawi la sanaa ambalo
linajishughulisha na kutafuta ukweli wa mambo jinsi yalivyo kwa njia ya fikra
na tafakuri za hali ya juu juu ya mambo hayo ambayo ni ukweli, mantiki, kuwepo
na kutokuwepo kwa mambo.
Baada ya kueleza maana ya Falsafa jinsi ilivyoelezwa hapo juu sasa
tuziangalie maana za miiko jinsi
zilivyojadiliwa navyanzo mbalimbali kama ifuatavyo;
en.wikipedia.org/wiki/Taboo Miiko ni makatazo makali ya matendo yaliyo
katika imani ya tabia ambayo pengine ni takatifu sana au laana sana kwa mtu
binafsi wa kawaida kufanya chini ya tishio ya adhabu isyo ya kawaida. (tafsiri
yetu)
www.wisegeek.com/what-is-a-taboo.htm Mwiko ni kukataza dhidi ya shughuli fulani, kwa kawaida mizizi katika
imani za kitamaduni au maadili. Vitu, watu, na maeneo pia
inaweza kama mwiko ilivyoelezwa,
kwa maana ya kuwa wao ni haramu au kwamba sheria
maalum zinazowazunguka wao.
www.oxforddictionaries.com/definition/english/taboo
Miiko kijamii au kidini
na desturi ni kukataza au kuzuia vitendo fulani au akipinga kushirikiana na mtu
fulani, mahali, au jambo.
Hivyo, miiko ni makatazo ambayo jamii huyaweka na kuyatilia adhabu kali
kwa mtu yeyote ambaye angeweza kukaidi maagizo hayo.
Baada ya kumaliza kueleza maana ya miiko sasa tuiangalie historia ya
wilaya ya Ukerewe ambamo ndimo miiko yetu tuliyoijadili ndimo
ilimotoka kama ifuatavyo;
https://envaya.org/lakevictoriachildren_lvc/history wanaeleza kuwa, Ukerewe ni kisiwa kubwa katika Ziwa
Victoria ambacho ni kubwa ya kitropiki na ni cha pili kwa ukubwa katika maziwa yenye maji baridi duniani. Kisiwa hiki kina ukubwa wa eneo la
6400 km2. nchi kavu ina 640 km2 ni nchi na wengine 5760 km2 ni maji ya
Ziwa Victoria Kuna visiwa 38 kisiwani Ukerewe kambapo makao makuu yake ni
wilaya ya Nansio . Kati ya visiwa 38,
visiwa 15 ni ya kudumu na hutumika kwa makazi wakati vinavyobaki hutumika kama
makazi yamda kwa wavuvi . Wilaya iko kusini mwa Wilaya Ilemela na Magu.
Mashariki kuna Wilaya Bunda na Musoma
katika Mkoa wa Mara, kwa kusini magharibi inapakana na Wilaya ya Sengerema, kwa
magharibi mkoa wa Kagera na kaskazini Jamhuri ya Kenya na Uganda
baada ya kumaliza kueleza historia ya
wilaya ya ukerewe ifuatayo ni miiko inayopatikana katika wilaya ya ukerewe
katika kabila la wakerewe.
1)
Nimarufuku kwa mtoto wa kiume kukaa
jikoni, maana yake ni kuwa, nguo za mama yake zinaweza kuvuka akaona uchi wa
mama yake. Lakini maana yake halisi ni kuwa kama mtoto wa kiume angekaa jikoni
angeliweza kuunguo
2)
Nimarufuku kuua chatu. Maana yake kwani
ni unauugua bila kupona na hadi kufa. Lakini ni kwamba chatu alikuwa amefugwa
na mtemi wa wakerewe.
3)
Nimarufuku mwanamke kutaja baba mkwe
wake kwa jina lake au jina linalofanana na la baba mkwe wake. Maana yake ni
kutunza heshima na badala yake mwanamke alitafta tafsida ya jina hilo ndiopo
amuite baba mkwe wake.
4)
Nimarufuku kwa mtu yeyote kuanza
kuchimba kaburi la mtualiyefariki mwenye
magonjwa kama kifafa, kichaa mpaka ndugu
yake aanza kuchimba ndipo wengine wafuatie. Hii ikikiukwa watu hao
watauugua mpaka kufa. Na suluhu yake ni
kwamba mazindiko hufanywa ili kuhakikisha marehemu anazikwa na magonjwa yake.
5)
Nimarufuku kwa bibi harusi kukatisha
katikati ya uwanja wa kaya. Hii ni kwa sababu katikati ya uwanja ndipo baba
nyenywe nyumba alipokuwa akiotea moto kwa hiyo angeliweza kumuona akiwa uchi.
6)
Nimwiko kwa mwanamke aliyeolewa kula na
baba mkwe wake meza moja. Hii ilikuwa ni
kwa sababu wanaume wanakula haraka na wanawake wanakula taratibu hivyo
waliogopa mkwe wao kutokushiba.
7)
Nimwiko kwa mwanamke kula nyama ya kuku
au mayai yake kwa kuogopa kuwa watoto wangekuwa na tabia za kula kila kaya.
Lakini maana yake ya ndani ni kuwa; kwakuwa wakerewe ni wafugaji wa kuku kwahiyo waliogopa kuku wao kumalizwa
na mama wakati wa ujauzito.
8)
Nimarufuku kwa mtoto yeyote kukalia kinu kama akikalia kinu
hatakua lakini maana yake ni kwamba ikiwa mtoto akikalia kinu angeweza kutoa
ushuzi na hatimaye kuchafua kinu ambacho ni chombo cha kutwangia nafaka.
9)
Nimarufuku kwa mwanaume kula na mama
mkwe wako. Kwani angweza kumlaza njaa lakini maana yake ni kwa nguo za mama
mkwe wake zingeweza kuanguka na kumuona uchi wake.
10)
Nimarufuku kwa wanaume katika familia
kula meza moja na wanawake kwani nguo zingaliweza kuanguka na kuwaona dada zake
na mama zake uchi. Lakini ni kwamba mwanamke anakula taratibu na mwanaume
anakula haraka haraka hivyo waliogopa kuwalaza njaa wanawake.
11)
Nimarufuku kwa mkerewe kula ndege aina
ya nfunzi kwani ataugua ugonjwa wa
kuvuka ngozi ya juu na ngozi ya ndani kuja juu. Lakini maana yake ni kuwa kwa
kuwa ndege huyo alikuwa natumika katika kufanyia shughuli za kiganga hivyo
waliogopa kuruhusu ndege hao wasilike ili wasije wakaisha mana hata upatikanaji
wake ni adimu sana.
Kwa
kuhitimisha tunaweza kutoa tathimini ya miiko hiyo na jinsi ilivyo kwa sasa.
Mpaka kufikia mwanzoni mwa miaka ya tisini miiko ilikuwa bado ina mashiko na
ilikuwa ikifanya kazi na watu waliieheshimu. Lakini baada ya kuingia kwa
maendeleo ya sayansi na teknolojia yaliyosukumwa na utandawazi miiko mingi ya
wabantu imekufa kwa kuwa mambo siku hizi yanapelekwa kizungu na kwa hali hii
kuna hatari ya miiko kufa na kupotea kabisa . hivyo juhudi za ziada
zinahitajika sana ili kuweza kuzilithisha katika vizazi vijavyo kwa kuanzisha miradi
mbalimbali ya kuandika miiko ili kuzitunza kwa mstakabali wa maisha ya baadaye.
MAREJELEO
http://pengotz.blogspot.com/2007/12/falsafa-ya-elimu-tanzania.html
imepakuliwa tarehe 13/04/2015 saa 4:48 asubuhi
en.wikipedia.org/wiki/Tabo imepakuliwa tarehe 14/04/2015
saa 2:16 usiku
http://sw.wikipedia.org/wiki/Falsafa. Imepakuliwa tarehe 13/04/2015 saa
4:18 asubuhi
Ijumaa, 9 Januari 2015
KATEGORIA ZA KISARUFI KWA MKABALA WA KIMAPIKEO
KATEGORIA ZA KISARUFI KWA MKABALA WA KIMAPIKEO
Dhana
ya kategoria ya kisarufi ni dhana telezi na ina ukakasi katika kuieleza licha
ya uwepo wa wataalamu mbalimbali ambao
wamejaribu kuifasili. Katika kujibu swali hili tutaanza kueleza maana ya
kategoria jinsi ilivyoelezwa na wataalamu mbalimbali, tutaeleza maana ya
kategoria ya kisarufi, vilevile tutaelezea dhana ya sarufi mapokeo tukihusisha
mawazo ya wataalamu mbalimbali, pia
tutadadavua kategoria ya kisarufi kwa mkabala wa sarufi mapokeo hatimaye
tutahitimisha kwa kueleza faida na hasara za sarufi mapokeo.
Kwa
kuanza, tuijadili dhana ya kategoria ya kisarufi jinsi ilivyojadiliwa na
wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo;
Zabroni (2013); anaeleza kuwa, kategoria
ni sifa zinazoambikwa katika aina mbalimbali za maneno.
Chombozi. Blogspot.com; waeleza
kuwa, kategoria ni aina za maneno kadri ya uainisho wake kutegemeana na sifa za
maneno husika kuwekwa katika kundi moja.
Matinde (2012); wanaeleza kuwa,
kategoria ni jumla ya maumbo, faridi na vipashio vilivyo katika hadhi sawa na huchangia sifa fulani katika tungo.
Hivyo, tunaweza kueleza kuwa
kategoria ni maumbo au vipashio mbalimbali vya kisarufi vinavyotumika
kubainisha mahusiano ya maneno katika tungo mbalimbali za lugha.
Baada ya kupata uelewa juu ya dhana
ya kategoria kama ilivyoelezwa na wataalamu mbalimbali, sasa tujadili dhana ya
kategoria ya kisarufi huku tukihusisha mawazo yetu na mawazo ya wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo;
www.out.ac.tz;
wanaeleza kuwa, kategoria
ya kisarufi ni kundi la maneno lenye sifa za kisarufi zinazofanana.
Matinde (2012: 187); anaeleza kuwa, kategoria za kisarufi ni maumbo
au vipashio vya kisarufi vinavyotumika kubainisha mahusiano ya kategoria za
maneno katika sentensi.
www.
Englishclub.com; wanaeleza kuwa,
kategoria za kisarufi (grammatical category) inahusu sifa maalumu ya neno
ambayo inaweza kusababisha kwamba neno
au maneno kuhusiana
na mabadiliko katika mfumo wa kisarufi. ( tafsiri yetu)
www.thefreedictionary.com; wanaeleza kuwa,
kategoria za kisarufi ni aina za maneno yenye sifa za kisarufi zinazofanana.
Kwahiyo tunaweza
kusema kwamba, kategoria za kisarufi ni sifa ya kitu (maneno au neno) ndani ya
sarufi ya lugha.
Baada ya kueleza
maana ya kategoria ya kisarufi jinsi livyoelezwa na wataalamu mbalimbali na vyanzo
vingine. Sasa tuieleze dhana ya sarufi mapokeo huku tukihusisha mawazo ya wataalamu
mbalimbali kama ifuatavyo;
Massamba na wenzake (1999);
wanafafanua kuwa sarufi mapokeo ni sarufi elekezi ilisisitiza usahihi wa lugha
kwa kuonyesha sheria ambazo hazina budi kufuatwa, mathalani, kufanya muundo
fulani wa sentensi uonekana kuwa sahihi,
au sheria ambazo hazina budi kufuatwa
ili kufanya matamshi ya neno fulani yakubalike kuwa ndio sahihi. Sarufi hizo za kimapokeo zilikuwa zikisisitiza jinsi
ambavyo lugha haikupaswa kuwa.
Kwahali hiyo; tunaweza kusema kuwa,
sarufi mapokeo ni sarufi ya kale ambayo ilionekana kutokuwa na msimamo wa Kisayansi
katika kuelezea lugha bali ilikuwa na mwelekeo wa kifalsafa na kujikita katika
kutambulisha kategoria mbalimbali za kisarufi ambazo zinatumika hadi hivi sasa.
Baada ya kumaliza kujadili maana ya
sarufi mapokeo; sasa tuzigeukie
kategoria za kisarufi kwa mujibu wa mkabala wa sarufi mapokeo ,
Kategoria ya nafsi; hii ni kategoria
ya sarufi mapokeo ambayo huelezea viwakilishi vya matenda/ mtendwa ambavyo
huambikwa kwenye vitenzi.Jedwali lifuatalo linaoneshsa kategoria za nafsi tatu ambazo pia zinaonekana
katika maumbo ya umoja na wingi zikiwa na viambishi vipatanishi vyake.
Nafsi
|
Umoja
|
Viambishi vipatanishi
|
Wingi
|
Viambishi vipatanishi
|
I
|
Mimi
|
Ni-
|
Sisi
|
Tu -
|
II
|
Wewe
|
U -
|
Ninyi
|
M -
|
III
|
Yeye
|
A -
|
Wao
|
Wa -
|
Mfano wa utokeaji wa nafsi katika
tungo;
(i)
Ni-, hii huonesha nafsi ya kwanza .
Mfano; Mimi ninakula. (umoja)
Sisi tunakula. (wingi)
(ii)
U-,
hii
huonesha nafsi ya pili .
(iii)
Mfano:
Juma unakula? (umoja)
Juma mnakula? (wingi)
(iv)
A-, hii hueonesha nafsi ya tatu .
Mfano: Mtoto anakimbia. (umoja)
Watoto wanakimbia.
(wingi)
Kategoria ya njeo. ni kategoria ya kisarufi mapokeo
ambayo huonesha na kuelezea tendo linavyotendeka ,lilivyotendeka na litakavyotendeka.
Katika lugha ya Kiswahili kategoria za njeo huwakilishwa na viambishi vitatu
ambavyo ni; -na-, -li-, na –ta-.
(a) –na- katika kuonesha wakati uliopo
Mfano, Wanatembea.
Anakula.
(b) –li- hii huonesha wakati uliopita
Mfano, Watoto
walicheza mpira.
Walimu walifundisha.
(c) -ta- hii huonesha wakati ujao
katika tungo.
Mfano, Mwalimu atafundisha kesho.
Rehema atarudi wiki ijayo.
Kategoria ya idadi. Hii ni kategora ya sarufi mapokeo
ambayo huonesha idadi katika tungo zinazohusu umoja na wingi. Mara nyingi
huonekana katika nomino na aina zingine za maneno kama vile vitenzi na vivumishi.
Mfano.
(a)
Mtoto anakimbia.
(umoja)
Watoto wanakimbia . (wingi)
(b)
Msichana mzuri . (umoja)
Wasichana wazuri.
(wingi)
Kwa kurejerea mifano hii
viambishi m- na wa-
kwa pamoja ni kategoria za idadi.
Kategoria ya hali. Hii ni kategoria ya kisarufi
mapokeo ambayo huelezea utendekaji wa
lile tendo ambalo lawezakuwa katika hali timilifu yenye kiambishi -me-
au hali ya mazoea yenye kiambishi hu-
Mfano; -me- katika hali timilifu
(a) Mwanaidi ametoroka nyumbani.
(b) Mwalimu amefundisha kiswahili.
(c) Juma amekimbia kichakani.
Mfano; hu-
katika hali ya mazoea
(a) Mutta hufundisha Kiswahili.
(b) Tababa hutembea harakaharaka.
Kategoria ya jinsia; hii ni aina ya kategoria ya kisarufi
mapokeo ambayo hubainisha maumbile katika tungo. Zipo jinsia za aina mbili.
(a) Jinsia ya kibaiolojia
(b) Jinsia ya kisarufi
(a) Jinsia ya kibaiolojia; hii ni aina
ya jinsia inayohusu maumbile ya mtu .Aina
hii husawiriwa na lugha. Aidha katika
lugha ya Kiingereza maneno kama Patron, He, Boy na Headmaster hudokeza jinsia
ya kiume ilhali yale ya Matron, She, Girl na Headmistress hudokeza jinsi ya
kike.
(b) Jinsia ya kisarufi; udhihilishwa na
maneno ya augha kuwekwa kwenye makundi bila kuzingatia kigezo cha kibaiolojia.
Hata hivyo, baadhi ya nomino katika lugha ya Kiswahili mfano; msichana,
mvulana, bibi, Baba , mama, kaka, dada na babu hudokeza jinsia.
Kategoria ya dhamira. Mtei (2008
uk.140); anaeleza kategoria ya dhamira na kuanza na fasili ya dhamira kuwa ni
kipengere cha kisarufi na kimaana ambacho huonesha lengo/ maana/
mwelekeo inayoiburiwa na vitenzi mbalimbali katika sentensi. Baada ya fasili
hii amabainisha aina za dhamira kama ifuatavyo;
(a) Dhamira elezi/ arifu; hii hutumiwa kueleza ukweli wa mambo jinsi ulivyo
vilevile hutoa taarifa kuhusu jambo.
Mfano, (i)
Mzozo huu umetatuliwa.
(ii) Mwizi yule alikamatwa.
(b) Dhamira amrishi; anaieleza kuwa
nidhamira ambayo hutumiwa kuonesha amri, ombi/ kutahadharisha.
Mfano, (i)
Simama juu.
(ii) Lete hilo jembe.
© Dhamira tegemezi; hii hutumiwa
kuonesha hali ya kutokuwa na hakika au uwezekano wa mambo au kutokea kwa matukio
.
Mfano,
(i) kutokuwa na hakika.
(a) Labda hakupata taarifa zako.
(b) Ikiwezekana nitakuja nae.
(ii) kutegemea kwa matukio.
Mfano,
(a) Mwalimu angenipa mtihani wangu
ningeweza kufanya masahihisho.
(b) Shule zikiongezeka watoto wengi watapata
elimu.
(iii) uwezekano wa jambo.
Mfano, (a) Mvua ingenyesha asubuhi tu.
(b) uzembe wake ungedhibitiwa
mapema.
Kategoria
ya kauli; katika kufafanua dhana hii Matinde (2012:190-205) anaeleza dhana ya
kauli kuwa, ni kategoria ya kisarufi ambayo uamilifu wake umekitwa katika kitenzi. Pia amezibainisha kauli mbalimbali
zinazojitokeza katika lugha ya Kiswahili kama ifuatavyo;
I.
Kauli ya kutendwa; hii ni kauli ambayo hubainisha kuwa kiima ni mtendewa au
mtendwa.
Mfano, (i) Uwanja umefyekwa.
(ii) Nyumba
imechomwa.
II.
Kauli tendi; hii ni kauli ambayo
hubainisha kuwa kiima ni mtenda. Kauli hii
huonyesha kuwa nomino iliyopo kwenye kiima ndiyo; ilitenda, itatenda, au
inatenda kitendo husika katika tungo.
Mfano.
(i) Mwajuma alipanda maboga.
(ii)
Mwalimu anafundisha.
III. Kauli ya kutendeka; hii haioneshi
uhusiano ulio wazi baina ya kiima na yambwa. Hata hivyo, kiima hupata
athari kutokana na kitendo husika. Katika kauli hii alomofu zinazoonesha kauli
hii ni {-ik-}, {-ek-}, {-lik-}, {-lek-}, {-ikan-} na {-eken-}.
Mfano,
(i) Nyumba inaanguka.
(ii) Kiti kimevunjika.
(iii) Fanyika
(iv) Vukika
(v) Tosheka
(vii) Ngoma hiyo haikututeka.
V.
Kauli ya kutendewa; hii hujumuisha
vitenzi vinavyotokana na kauli ya kutendea kuongezewa viambishi. Alomofu zake
ni {–w-}, {-liw-}, {-iw-} au {-ew-}
Mfano,
(i) Pigwa
(ii) Cholewa
(iii) Imbiwa
VI.
Kauli ya kutendeka; hii ni kauli ambayo
huonesha jinsi jambo linavyotendeka. Alomofu zinazobainishwa katika kauli hii
ni {-ek-}, {-ik-}, {-lik-}
{-elek-}, {-ikan-}, na {-iken-}.
Mfano; (i) pigika
(ii) chezeka
(iii) Someka
VII.
Kauli ya kutendua; kauli hii
hudhihirishwa na kinyume cha utenduzi. Alomofu za kauli hii ni. {-u-}, {-a-},
{-i}, {-e-}.
Mfano: (i) Fungua
(Ii) Umbua
(Iii) Chomoa
VIII. Kauli
ya kutendana; hii ni kauli ambayo hubainisha
uhusiano fulani kati ya kiima na yambwa. Alomofu za kauli hii ni {-an-}
Mfano.
(i) Sukana
(ii) Chekana
(iii) Somana
IX.
Kauli ya kutendesha; hii ni kauli ambayo
hubainisha dhana ya usababisho kati ya kiima na yambwa. Alomofu zinazojitokeza
katika kauli hii ni: {-esh-}, {-lesh-}, {-lish}, {-ez-}, {-iz-} ambazo
hutegemea vitenzi husika katika tungo.
Mfano; (i) Ogesha
(ii) Pigisha
(iii) Chezesha
Kategoria ya uhusika;
Matinde (2012:207), ameeleza uhusika kuwa ni kategoria ya kisarufi ambayo
huonyesha uhusiano wa viambajengo katika tungo. Aidha huonyesha uamilifu wa
kila kiambajengo katika tungo na athari ya kila kiambajengo hicho kwa
viambajengo vingine. Uhusika huu huweza kugawanyika katika aina sita kama
ifuatavyo;
(i)
Uhusika wa kiima; huu hubainisha kuwa
nomino, au kiwakilishi chake huchukua nafasi ya kiima.
Mfano: (a) Daktari
alimkaribisha mgonjwa.
(b) Musa
amejengewa nyumba .
(ii) Uhusika
tendea; uhusika huu huonyesha kuwa nomino au kiwakilishi chake kinathirika kutokana na tendo fulani.
Mfano: (a) Mwiba
ulimchoma Jeska.
(b) Yeye alifukuzwa na mwalimu.
(iii)
Uhusika ala; huu huonesha kitu ambacho hakina hisia kilichotumika katika kutekeleza kitendo au jambo fulani.
Kifaa hiki hutumika kusababisha utokeaji wa tendo au hali ambayo inadokezwa na
kitenzi.
Mfano: (a)
Alivunja mlango kwa nyundo.
(b) Alimkata kwa panga.
(iv)
Uhusika yambwa; huu huonyesha kuwa nomino au kiwakilishi chake kimechukua
nafasi ya yambwa katika tungo.
Mfano: (a) Jumanne alinunuliwa baisikeli.
(a)
Mfano: Mwanafunzi aliyefauru vizuri
awazawdiwa daftari.
(v)
Uhusika mahali; huu hubainisha mahali au mwelekeo wa kieneo wa hali au tendo
ambalo linadokezwa na kitenzi.
Mfano: (a) Mbwa yuko nyuma ya kabati.
(b) Ameweka jagi chini ya meza.
(vi)
Uhusika mtendwa au mtendewa; huu
hudhihirisha kiumbe chenye hisia ambacho kinathirika na hali au tendo
linalodokezwa na kitenzi.
Mfano: (a) Mtoto aliangushwa naa mbuzi wake.
(b) Yule msichana amechomwa na mwiba.
Kategoria ya ngeli;
Wahiga (1999:40), analeza maana ya ngeli kuwa ni jamii ya nomino zenye kuleta
mabadiliko ya aina moja ya viambishi vya maneno katika umbo la umoja na wingi. Masebo
na wenzake (2003) wanaeleza kuwa, huu ni mtazamo mkongwe zaidi uliofuatwa na
wanasarufi mapokeo ambao miangoni mwao alikuwa ni Meinholf baadaye akafuatwa na
Broomfeld (1931) na Ashitoni (1944) ambao waliziainisha nomino kulingana na
viambishi awali vya nomino. Nomino zote zilizokuwa na viambishi vinavyofanana
ziliwekwa katika kundi moja na kufanya ngeli moja.
Mfano
ni katika jedwali lifuatalo;
|
Ngeli
|
Viambishi
awali vipatanishi
|
Mifano
|
1
|
A-WA
|
A- Umoja
WA-
wingi
|
Mtoto
anakuja - watoto wanakuja
Mwalimu
ameondoka - walimu wameondoka
|
2
|
U-I
|
U-
umoja
I-wingi
|
Mmea
umenyauka - mimea imenyauka
Mkungu
umenunuliwa - mikungu imenunuliwa
|
3
|
LI-YA
|
LI-Umoja
YA-
wingi
|
Yai
limepasuka - mayai yamepasuka
Embe
limeoza - maembe yameoza
|
4
|
KI-VI
|
KI-
Umoja
VI-
Wingi
|
Kiti
kimevunjika - viti vimevunjika
Kikombe
kimekatika - vikombe vimekatika
|
5
|
I-ZI
|
I-umoja
ZI-
wingi
|
Nyanya
imechumwa - nyanya zimechumwa
Soda
imeuzwa - soda zimeuzwa
|
6
|
U-ZI
|
U-
umoja
ZI-wingi
|
Ufunguo
umepotea - funguo zimepotea.
Uzi
umenunuliwa - nyuzi zimenunuliwa.
|
7
|
U-YA
|
U-
Umoja
YA-
wingi
|
Ugonjwa
umeenea - magonjwa yameenea
Uasi
umeisha - maasi yameisha
|
8
|
KU
|
KU-
Umoja
|
Kusuka
kunachosha
Kuigiza
kunaburudisha
|
9
|
PA-MU-KU
|
PA-umoja
MU-Umoja
KU-
umoja
|
PA-
Mahali hapa pananuka
MU-
Mahali humu munamaji
KU-
Mahali kule kuna giza.
|
Kwa
hiyo, licha ya wanasarufi mapokeo kutumia lugha ya kilatini kama kigezo cha
kupima ubora wa lugha kuwa ni makosa kwa sababu ya kuwa kila lugha ina mtindo
wa kipekee wa kuunda tungo zake, lakini faida kubwa inayojitokeza kwa
wanasarufi mapokeo ni kuwa waliweza kuanzisha kategoria mbalimbali za kisarufi
ambazo zinatumika mpaka sasa katika uga wa sarufi.
MAREJELEO
Masebo na wenzake, (2002). Kiswahili
Kidato cha 3 na 4. Nyambari Nyangwine Publishers:
Dar es Salaam.
Massamba na wenzake, (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA). TUKI:
Dar es Salaam.
Matei, A. K. (2008). Darubini ya Sarufi. Phoenix Publishers: Nairobi.
Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha; Isimu na Nadharia. Serengeti Educational
Publishers
(T)
Limited: Mwanza.
Philipo, Z. (2013). Sintaksia ya Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dodoma: Dodoma.
Waihiga, G. (1999). Sarufi Fafanuzi ya Kiswahili. Longhorn Publishers: Nairobi.
www.chombozi.blogspot.com.
(Ilitembelewa tarehe 23/12/2014 saa 04:30 usiku.)
www.englishclub.com.
(Ilitembelewa tarehe 23/12/2014 saa 05:45 usiku.)
www.out.ac.tz.
(Ilitembelewa tarehe 23/12/2014 saa 05:50 usiku.)
www.thefreedictionary.com.
(Ilitembelewa tarehe 24/12/2014 saa 07:01 usiku.)
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)