Jumamosi, 13 Desemba 2014

NADHARIA NA MBINU ZA TAFSIRI




 
RICHARD, KASHINJE NDIYE MWANZILISHI NA MWANDISHI WA BLOG HII

HISTORIA YA TAFSIRI
Historia na maendeleo ya tafsiri ulimwenguni imeelezwa na wataalamu mbalimbali ambao ni kama vile Mwansoko na wenzake (2006), Wanjala (2011), Mshindo (2010), Sofer (2006) ambapo wataalamu hawa wamegawa historia na maendeleo ya tafsiri katika vipindi vifuatavyo:

Enzi za kale. Kipindi hiki kinajumuisha wakati wote wa kihistoria kati ya mwaka 300KK hadi 300BK. Hiki ni kipindi ambacho kilikuwa na maendeleo ya sayansi na taaluma nyingi za kisasa ambapo zinasadikika zilianzia huko Misri. Ugunduzi na ustaarabu ulioletwa na wamisri uliigwa na wayunani na kuwa chimbuko la ustaarabu wa ulaya. Mbinu iliyotumika na wayunani kuchota maarifa ya wamisri ni tafsiri. Wayunani walikaa misri kwa muda na kujifunza lugha ya wamisri na elimu yao. Mambo waliojifunza waliyafasiri kwa kiyunani na kwenda kuyasambaza huko ulaya.

Enzi za giza. Hiki ni kipindi kati ya karne ya 5 hadi 11. Kipindi hiki kiliitwa kipindi cha giza kwasababu kilitawaliwa na misingi ya utamaduni kuoza na uozo wa kijamii kukita mizizi ambapo mambo kama ubashi, ukahaba na unajisi vilikithiri, pia shughuli za elimu zilikwama huko ulaya. Katika kipindi hiki kulikuwa na mapigano kati ya waislamu na wakristo ambapo baada ya mapigano hayo maarifa ya wagiriki yaliyosheheni ujuzi wa sayansi yalifasiriwa kwa kiarabu. Pia baadhi ya mataifa mfano Hispania yalichukua vitabu ambapo vilikuwa vimesheni maarifa ya sayansi na kuyapeleka kwao na kutafsiri katika lugha zao. Tafsiri hizo zilipelekea ulaya kutoka katika kipindi cha giza na kuingia katika kipindi cha ufufuko wa elimu na maarifa. (Renaissance)

Enzi za ufufuko. (Renaissance) inamaana ya ufufuko wa hamu kuu ya elimu na maarifa. Kipindi hiki kilivuma sana ulaya kusini hasa Italia kikiwa na lengo la kufufua shughuli za elimu na utamaduni. Wazungu walipofika Uarabuni walistaajabia elimu ya kisayansi wakayachukua maarifa hayo na kuyafasiri katika lugha mbalimbali mfano kifaransa, kijerumani na kiingereza. Fasili hizo zilizua msisimko wa shughuli za kielimu, maarifa na utamaduni.

Enzi za kati. Hiki ni kipindi kilichoonesha muamko wa kidini katika karne ya 16 ambapo ilianza ujerumani na kusambaa katika maeneo mengine ulimwenguni. Mwamko huu ulipinga muundo, mwelekeo, falsafa na mafunzo mengi ya kanisa katoliki ya wakati huo na matumizi ya lugha moja ya kilatini katika misa na mafunzo. Hali hii ilisababisha mgawanyiko katika dini ya kikristo, watu mbalimbali walitafsiri maandiko matakatifu katika lugha mbalimbali kwa mfano Martin Luther King alitafsiri biblia takatifu kutoka kilatini kwenda kiingereza (1611) ikaitwa The King James Bible, pia alitafsiri biblia kutoka kilatini kwenda lugha ya kijerumani. Baada ya kuona tafsiri ya kilatini imeacha baadhi ya vipengele katika maandiko hayo matakatifu . Jarome alitafsiri biblia ya kigiriki na kiebrania kutoka kwenye lugha ya kilatini

Enzi za kisasa. Kipindi hiki kilikuwepo karne ya 20 ambapo kilijulikana kama kipindi cha tafsiri kutokana na wingi au mfumuko wa tafsiri. Kipindi hiki kimetawaliwa na masafa marefu ya mawasiliano, maendeleo makubwa ya kielimu na ethnolojia, utandawazi na usomi wa lugha, isimu na fasihi. Mikataba ya kimataifa baina ya mashirika ya umma na ya binafsi inafasiriwa kwa yeyote anayehitaji taarifa hizo. Tafsiri ilikolea katika karne hii kutokana na kuzuka kwa mataifa mengi huru yanayoteua lugha rasmi, lugha za taifa na lugha za elimu.

Kwa hiyo baada ya hitaji kubwa la watu kutaka kuwasiliana na jamii au watu wa mataifa, kabila tofauti. Kutokana na hitaji lake kubwa hilo imepelekea taaluma hii kukuwa kwa kasi sana ukilinganisha kipindi cha nyuma  hasa baada ya mapinduzi ya viwanda karne ya 18.
Baada ya kujadili historia na mandeleo ya tafsiri ulimwenguni, sasa tunaweza kujadili historia na maendeleo ya tafsiri nchini Tanzania.

Kwa ujumla historia na maendeleo ya tafsiri nchini Tanzania haina historia ndefu sana kwani inaanzia mnamo karne ya 19 ambapo tunaweza kugawa historia na maendeleo haya katika vipindi vitatu ambavyo, ni kabla ya utawala wa kikoloni, wakati wa utawala wa kikoloni na baada ya uhuru.
Kabla ya utawala wa kikoloni, wamisionari walitafsiri vitabu mbalimbali vya kikristo ikiwemo biblia takatifu kutoka lugha ya kiingereza kwenda Kiswahili na lugha nyingine za makabila kwa lengo la kueneza dini na ustaarabu wa kikristo kwa waafrika.

Wakati wa utawala wa kikoloni, hiki ni kipindi kuanzia miaka ya 1800, katika kipindi hiki wakoloni hasa waingereza walitafsiri maandiko mbalimbali ya kitaaluma na fasihi ya Ulaya kwa lugha ya Kiswahili. Mfano Pia kabla ya uhuru baadhi ya kazi za fasihi zilitafsiriwa kwa mfano tamthiliya ya Mzimu wa Watu wa Kale iliyotafsiriwa na Mohamed S. Abdalla (1960) kutoka lugha ya kiingereza (Shrine of The Ancestors).

Baada ya uhuru ambayo ni kuanzia mwaka 1961, katika kipindi hiki wapo wataalamu waliofanya juhudi za kutafsiri vitabu mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili mfano mzuri ni Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye alitafsiri vitabu viwili vya mwandishi mashuhuri wa tamthiliya wa huko Uingereza William Shakespeare ambavyo ni tamthiliya ya Juliasi Kaizari (Julius Caesar) (1963) na tamthiliya ya Mabepari wa Venis (The Merchant of Venis) (1969).

Kazi nyingine zilizotafsiriwa baada ya ukoloni ni pamoja na ushairi wa Wimbo wa Lawino iliyotafsiriwa na Paul Sozigwa (1975), kutoka lugha ya kiingereza (Song of Lawino), riwaya ya Uhuru wa Watumwa iliyotafsiriwa na East African Literature Bureau (1967) kutoka lugha ya kiingereza (The Freeing of The Slaves in East Africa). Pia kazi nyingine za fasihi ambazo zimetafasiriwa kwa lugha ya Kiswahili hapa Tanzania ni pamoja na Nitaolewa Nikipenda ambacho kimetafsiriwa na Crement M. Kabugi (1982) kutoka lugha ya kiingereza (I will marry when I Want).

Kwa sasa maendeleo ya taaluma ya tafsiri nchini Tanzania yamepiga hatua kubwa kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia. Taaluma ya tafsiri kwa sasa inafundishwa katika elimu ya sekondari na vyuo mbalimbali. Pia taasisi na asasi zinazojishughulisha na tafsiri zimeongezeka kwa mfano Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI), Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) na

NADHARIA MAHUSUSI ZA TAFSIRI.
1. Nadharia ya Usawe wa Kimuundo; nadharia hii inatetewa na mtaalam Catford (1969), Tunapofanya kazi ya kutafsiri tunatakiwa kuzingatia ulinganifu wa kimuundo kati ya matini chanzi na matini lengwa, maana yake ni kwamba muundo wa matini chanzi ujitokeze katika matini lengwa. katika nadharia hii muundo ni muhimu. Pia nadharia hii hutumika zaidi katika kutafsiri maandiko ya kidini hasa Biblia.
2. Nadharia ya Usawe wa Kidhima; wa tetezi wa nadharia hii ni pamoja na Nida (1964) na Nida na Taber (1969) wanaona kuwa usawe wa kidhima ni muhimu zaidi kuliko usawe wa kimuundo. Wafasiri wanapaswa kuhakikisha kwamba dhima ya matini chanzi pamoja na athari zake zinajitokeza katika matini lengwa. Yaani kama matini chanzi inawalenga watoto inapaswa iandikwe kiasi kwamba watoto wataweza kuelewa. Pia kwa kuzingatia nadharia hii unapaswa kutumia lugha rahisi na inayoeleweka na watu wote. Vilevile tafsiri yako iwe nzuri kiasi kwamba mtu atakaposoma asiweze kujua kwamba hii kazi imetafsiriwa.

3. Nadharia ya Usawe wa Aina-matini; matini yoyote ile ifasiriwe kwa kuzingatia aina yake. Hii inamaana kwamba kazi itakayotokea itafanana na matini chanzi. Kma matini chanzi ni ya kisheria itakapotafsiriwa matini lengwa nayo itaonekana kuwa ya kisheria. Katika nadharia hii kinachozingatiwa ni fani (muundo) na maudhui (dhima/lengo) ya matini yenyewe inayotafsiriwa. Watetezi wa nadharia hii ni Reiss (1971), Buhler (1965) na Newmark (1982/88)

4. Nadharia Changamani (Cross Fertilization theory). Hii ni nadharia tete iliyoasisiwa na P.S.Malangwa (2010) Ndharia hii inadai kwamba huwezi kufanya tafsiri kwa kutumia nadharia moja tu, kwa sababu hakuna nadharia inayojitosheleza yenyewe.

UAINISHAJI WA MTINI

Maana: Kuainisha matini ni kuzigawa au kuziweka matini katika makundi mbalimbali kwa kuzingatia kufanana kwake. Sababu: Tunaainisha matini kwa sababu kila matini inahitaji mbinu maalum ya kuitafsiri. Mikabala/vigezo vya uainishaji: Wataalam wengi wanatumia vigezo vitatu ambavyo ni Kigezo cha Mada (Topic/Field), Kigezo cha Matumizi ya Istilahi, Kigezo cha Dhima kuu za Lugha

1. Kigezo cha Mada: katika kigezo hiki tunaangalia maudhui ya jumla ya matini. Tunajiuliza matini hii inahusu uwanja gani hasa katika maisha? Kwa kutumia kigezo hiki cha mada tunapata aina tatu za matini. i) Matini za Kifasihi (Literary Text); hizi ni matini ambazo zinahusu fani mbalimbali za fasihi kama vile riwaya, tamthilia, ushairi nk. ii) Matini za Kiasasi (Institutional Texts); matini hizi ni mtini za kimamlaka kama vile matini za kisiasa na kiserikali (hotuba, risala, mikataba, vyeti nk). iii) Matini za Kisayansi (Scientific Texts); matini hizi hujumuisha masuala yote ya Sayansi na Teknolojia. Kwa mfano; Fizikia, Kemia, Biolojia nk.

2. Kigezo cha matumizi ya Istilahi: katika kigezo hiki kinachozingatiwa hapa ni kwamba, matini huainishwa kwa kuangalia wingi au idadi za istilahi-msamiati wa uwanja maalum/husika mf: sharia nk. Kwa kutumia kigezo hiki tunapata aina tatu za matini:
 a) Matini za kiufundi (Technical Text), matini hizi huwa na idadi kubwa ya istilahi.
 b) Matini za kinusu ufundi (Semi-Techinical Text), matini hizi huwa na idadi ndogo au chache za istilahi.
 c) Matini za zisizo za kiufundi (Non Techinical Text), matini hizi ni zile ambazo hazina kabisa istilahi bali hutumia maneno ya kawaida kabisa.

3. Kigezo cha Dhima Kuu za Lugha (Major Language Functions). Buhler (1965) alipendekeza dhima kuu 3 za lugha.
i) Dhima elezi (Expressive Function), katika dhima hii lugha hutumika kuelezea hisia za mwandishi/mzungumzaji. Anasema, mzungumzaji au mwandishi hueleza hisia zake bila kumjali msikilizaji au msomaji.
ii) Dhima Arifu (Informative Function), dhima hii ya lugha hujitokeza pale ambapo matini au lugha inatumika katika kutoa taarifa kuhusu jambo fulani. Dhima hii huegemea kwenye ukweli wa mambo.
iii) Dhima amili (Persuasive Function) katika dhima hii lugha hutumika kuchochea hisia za msikilizaji au msomaji. Kiini cha dhima hii ni hadhira. Kwa hiyo, kwa kuzingatia dhima hizi tatu “3” tunapata aina kuu tatu za matini kama ifuatavyo:
1.      Matini Elezi (Expressive Texts); matini hizi huegemea upande wa mwandishi. Mwandishi hutumia matini hizi kuelezea hisia zake. Mfano, kazi mbalimbali za kifasihi, hotuba, matini mbalimbali za kimamlaka, matini za kisheria, matini mbalimbali za kitaaluma, maandishi binafsi nk. 2.
2.       Matini Arifu (informative Texts); matini hizi ni zile ambazo zinatoa taarifa au maarifa kuhusu jambo fulani. Sifa yake ni kuwa zinakuwa na umbo sanifu au umbo maalum mfano; umbo la jarida, kitabu, ripoti, tasnifu, vitabu vya taaluma mbalimbali nk. 3. Matini Amili (Persuasive Texts); matini hizi huegemea upande wa hadhira. Katika matini Amili mwandishi hujitahidi kadiri awezavyo kuchochea hisia za wasomaji na kuwafanya watende kama ambavyo mwandishi anataka watende. Hivyo huegemea upande wa msomaji. Mfano wa matini hizo ni kama vile mialiko mbalimbali, matangazo, maelekezo mbalimbali nk.

UCHAMBUZI WA MATINI ZA TAFSIRI

Awali ya yote mchambuzi wa matini za tafsiri/mfasiri anapaswa kusoma matini kwa kina na kuyaelewa kabla ya kuanza zoezi zima la uchambuzi wa matini. Maana: Uchambuzi wa matini unatuwezesha kubaini sifa na vipengele vinavyojenga matini husika kimuundo, kidhima na kiitikadi. Hatua/vipengele vya uchambuzi wa matini: Uchambuzi wa matini unahatua tatu “3” ambazo ni kama ifuatavyo:
1. Kusoma matini yote na kuielewa vizuri. Hii humsaidia mfasiri kuweza kuandaa marejeleo muafaka, kuandaa vitabu au machapisho mbalimbali yatayomsaidia katika zoezi zima la kufasiri matini. Kwa mfano; - Kuandaa kamusi mbalimbali kama vile kamusi ya lugha chanzi, kamusi ya lugha lengwa, kamusi ya visawe, kamusi ya fani maalum. - Inamsaidia mfasiri kuandaa orodha ya istilahi. - Inamsaidia mfasiri kuweza kugawana sehemu au vipengele vya matini kwa wafasiri wengine.
2. Kuchambua matini yenyewe. Uchambuzi wa matini hulenga kupata nduni bainifu za matini husika (Distinctive Features). Kipengele hiki cha pili kina hatua ndogo ndogo tano ambazo ni kama ifuatavyo:
 a) Kubaini lengo la mwandishi wa matini chanzi. Mfano; malengo ya mwandishi huweza kuwa kukweza, kusifu, kukashfu au kuarifu jambo. Kwa kawaida waandishi wa matini chanzi wanakuwa na mitazamo mitatu;
i) Mtazamo hasi kwa mtendwa (biased) mfano, katika gazeti; “Chelsea yaichabanga Arsenal tatu nunge”
ii)Mtazamo chanya kwa mtendwa (biased) mfano katika gazeti; “Chelsea yafuta uteja kwa Arsenal”
 iii) Mtazamo wa kati (neutral) mfano katika gazeti; “Chelsea yaifunga Arsenal au Arsenal yafungwa na Chelsea”

 b) Kubaini lengo la mfasiri. Mfasiri anapaswa kujiuliza kwa nini nafasiri kazi hii? Je lengo langu na mimi ni tofauti na la mwandishi? - Aepuke upendeleo kwa hadhira chanzi na hadhira lengwa badala yake ajikite katika ukweli. Hivyo inafaa awe katika mtazamo wa kati (neutral) - Kama kuna haja ya kuegemea upande mmoja basi aegemee kwa hadhira lengwa.

 c) Kubaini hadhira na umbo la matini. Kwa mfano; kama matini chanzi ni kitabu basi matini lengwa nayo iwe kitabu.
 d) Kubaini mtindo wa matini. Hapa mfasiri ahakikishe kwamba mtindo wa matini chanzi unajitokeza katika matini lengwa. Mfano; kama kuna monolojia au dayalojia basi na matini lengwa inapaswa kuwa hivyo.

 e) Kubaini ubora na mamlaka ya matini chanzi. Hapa mfasiri hanabudi kuzingatia ujuzi wa mwandishi katika kutumia zana za kiisimu/vipengele mbalimbali vya lugha. Mamlaka hutokana na hadhi au ubobevu wa mwandishi huyo katika taaluma au fani aliyoandikia. Mfano, kazi ya fasihi ya S. Robert ni bora kuliko iliyoandikwa na mimi kwa sababu yeye ni mbobevu/galacha katika taaluma hiyo.

3. Kusoma matini kwa mara ya mwisho. Katika hatua hii ya tatu mfasiri asome tena matini chanzi ili kutoa taashira (highlight) kuhusu maneno au mambo muhimu. Mambo muhimu ni: Majina mahususi ya watu, mahali, sehemu au miaka, maeneo ambayo hayatafsiriki kirahisi ili aweze kuyashughulikia upya hapo baadaye.

MCHAKATO WA KUTAFSIRI/KUFASIRI
Hatua muhimu katika kutafsiri Tunapofanya tafsiri kuna hatua muhimu kuu sita kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2006). Hatua hizo ni kama ifuatavyo:
1. Hatua ya maandalizi. Hatua hii inahusisha mambo matatu ambayo ni:
a) Kupitia tena sehemu muhimu za matini chanzi, kwa mfano; istilahi, majina ya wahusika, majina ya kijiografia, maeneo au kauli zisizofasirika kirahisi.
b) Kupata marejeleo ili kutafuta visawe vya kisemantiki
 c) Kutafuta na kuandika visawe hivyo.

 2. Hatua ya pili baada ya maandalizi ni uhawilishaji (transferring/transference). Katika hatua hii mfasiri uhawilisha ile taarifa kutoka kwenye matini chanzi kwenda kwenye matini lengwa, hapa mfasiri anatakiwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa na lugha chanzi. mfano; “My new car is broken”-langu jipya gari ni vunjika. Tafsiri ya Kiswahili sanifu inapaswa kuwa “Gari langu jipya limeharibika” Uhawilishaji maana yake ni kuhamisha maana, ujumbe nk. kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa, lengo la matini au mwandishi, umbo la matini, mtindo nk. Mbinu ya tafsiri ambayo inatumika katika hatua hii ya uhawilishaji ni tafsiri ya neno kwa neno.

3. Hatua ya tatu ni kusawidi rasimu ya kwanza (drafting). Uhawilishaji wa visawe kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa unapokamilika kinachopatikana ni rasimu ya kwanza ya tafsiri. Rasimu ya kwanza ya tafsiri inakuwa na dosari nyingi na kwa hiyo haifai kupelekwa kwa mteja au hadhira. Badala yake rasimu ya kwanza lazima ipitiwe tena upya na kurekebishwa au kudurusiwa/durusu (review) rasimu (draft).

4. Hatua ya nne ni kudurusu rasimu ya kwanza ili kuunda rasimu ya pili. Mfasiri hupata fursa ya kwanza ya kuitathimini na kuifanyia marekebisho tafsiri yake mwenyewe. Kazi ya kudurusu haipaswi kufanywa haraka. Wataalam wengine kama vile Larson (1984) anasema rasimu ya kwanza ni lazima iachwe kwa muda wa wiki moja. Udurusu unahusisha shughuli zifuatazo: · Kusahihisha makosa ya kisarufi, miundo isiyoeleweka vizuri. · kunyoosha sehemu zenye tafsiri ya mzunguko na zenye matumizi potofu ya visawe. Mfano; “He rarely visits me these days – Siku hizi ni aghalabu-nadra sana yeye kunitembelea.” ·Kurekebisha sehemu zenye muunganiko tenge/mbaya ambazo zinazuia mtiririko mzuri wa matini. Kuhakiki usahihi na kukubalika kwa maana zinazowasilishwa katika matini lengwa. Hapa tunaangalia kama kuna mambo yameongezwa, yamepunguzwa au yamepotoshwa/kubadilishwa. ·Kuhakiki kukubalika kwa lugha uliyotumia katika tafsiri yako kwa kuzingatia umbo na mada ya matini chanzi. ·Kuona iwapo mada au ujumbe mkuu wa matini chanzi unajitokeza waziwazi katika matini lengwa.

5. Hatua ya tano ni kusomwa rasimu ya pili na mtu mwingine. Msomaji wa rasimu ya pili anaweza kuwa mfasiri au shabiki wa tafsiri, mhakiki au mhariri wa tafsiri anaweza kuwa mteja wa tafsiri husika au mtu mwingine yeyote unayemwamini. Namna ya kumpa mtu akusomee rasimu: · Kumpa bila kumjulisha kwamba ni tafsiri · Unampa matini chanzi na matini lengwa ili alinganishe. Inapendekezwa kwamba mtu huyo asome kwa sauti ili uweze kubaini mapungufu.

6. Hatua ya sita ni kusawidi rasimu ya mwisho. Katika hatua hii mfasiri atafanyiakazi maoni na mapendekezo ya msomaji ambaye alimpa kazi yake. Matokeo ya kufanyiakazi maoni ya mteja hutupelekea kupata rasimu ya mwisho ambayo ndiyo humfikia mteja, hadhira, wachapaji nk.


Maoni 30 :

  1. kazi nzuri ila tuongeze mawazo mengine kama mbinu za tafsiri na mengineyo yanayohusu tafsiri.

    JibuFuta
  2. Kazi nzuri, ina manufaa ajabu

    JibuFuta
  3. Juu mwongozo ni muhimu xana

    JibuFuta
  4. asante lakini jaribu kutupa mifano ya tafsiri kwenye nadharia

    JibuFuta
  5. Pongezi kwa kazi nzuri.. Jaribu kuandika kurasa ya marejeleo .

    JibuFuta
  6. Kazi nzuri sana. Hakikisha kwamba andiko lolote la kitaaluma linakuwa na marejeo kuwapa heshima wataalamu mbalimbali waliofanya kazi kubwa sana kweny uga wa kitaaluma.

    JibuFuta
  7. Heko! kwa kazi nzuri,ningependelea pia uongezee kwa kutuelezea Nadharia ya tafsiri kwa kuangalia
    1.Isumu linganishi
    2.Isimu jamii na
    3.Mawasiliano katika tafsiri.
    Shukran, ubarikiwe.

    JibuFuta
  8. kazi nimeipenda mungu akuzidishie

    JibuFuta
  9. Ni zipi nadharia za tafsiri?

    Shukrani.

    JibuFuta
  10. Kazi ni nzuri sana lakini haina marejeleo maana ake rukiiona tunasema umebuni mwenyewe kitu ambacho ndivyo sivyo

    JibuFuta
  11. Kazi nzuri lkn tungepata na sababu za Kuanzishwa kwa Tafsiri zisipungue 5

    JibuFuta